WAKAZI wa Mbagala jijini Dar es Salaam watapata neema mbili mwakani baada ya serikali kutangaza kuanza awamu ya pili ya ujenzi wa mradi huo, lakini pia uwapo wa fidia kwa wenye nyumba ambazo zitabomolewa ili kupisha ujenzi wa miundombinu yake.


Awamu ya pili ya mradi huo itaanzia Gerezani hadi Mbagala Rangi Tatu.

Baada ya kukamilika kwa awamu ya kwanza ya mradi huo imeelezwa kuwa awamu ya pili inatarajiwa kuanza Juni mwakani ikihusisha Barabara ya Kilwa kutoka Gerezani hadi Mbagala Rangi Tatu ikitarajiwa kugharimu Sh. bilioni 360.

Akizungumza na Nipashe kwa simu mwishoni mwa wiki iliyopita, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart), Ronald Rwakatare, alisema zabuni ya kumpata mkandarasi wa ujenzi huo inatarajiwa kutangazwa mwezi ujao.

Alisema Sh. bilioni 360 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi huo na kati yake, kuna kiasi kwa ajili ya ulipaji fidia kwa wamiliki watakaobomolewa nyumba zao.

Hata hivyo, Rwakatare hakuwa tayari kutaja kiasi halisi kilichotengwa kufidia wamiliki hao kwa kuwa Mthamini Mkuu wa Serikali bado hajakamilisha kazi yake.

"Hicho kiasi cha fedha tumeomba kwa ajili ya barabara hiyo," Rwakatare alisema. "Bado tathmini inaendelea. Kwa hiyo ndiyo 'figure' (kiasi) tuliyotenga kwenye bajeti lakini bado kuna kiasi kingine kitaongezeka.

"Kuna fedha imetengwa kwa ajili ya fidia, lakini siwezi kuizungumzia kwa sasa kwa sababu Mthamini Mkuu wa Serikali bado hajakamilisha kazi yake. Pindi atakapokamilisha tutasema ni kiasi gani kimetengwa kwa ajili ya fidia."

MKUSANYA NAULI

Wakati huo huo, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart), Ronald Rwakatare, amesema mchakato wa kumtafuta mzabuni wa kusimamia utengenezaji wa kadi za abiria wa mabasi hayo unaendelea.

"Tumechelewa kutoa kadi zingine kwa sababu sasa hivi tunamtafuta mtu ambaye ni mkusanya nauli kwa njia ya zabuni. Mara tutakapompata ndio huyo tunategemea ataleta kadi na kuongeza zingine," alisema.

Kumekuwa na usumbufu kwa abiria wengi kulazimika kukaa foleni ndefu kusubiri kukata tiketi za mabasi hayo ambayo wakati huduma zake zikianza nchini Mei, mwaka jana ilielezwa kuwa zingetumia kadi za kielektroniki zaidi.Alibainisha kuwa awali walitoa kadi 200,000 ambazo zilitumika katika kipindi cha mpito na zote zilichukuliwa haraka na wananchi.

"Ilikuwa huduma ya mpito," alisema, "haikuwa huduma kamili. Tukipata huyo mzabuni kwa njia ya ushindani ndio tutapata kadi kamili zinazohitajika. Lazima tupitie mchakato wa zabuni, ili apatikane aweze kutoa kadi zingine."Mwanzoni mwa mwaka huu, Rais John Magufuli alifungua rasmi awamu ya kwanza ya miundombinu na utoaji huduma ya mabasi hayo iliogharimu Sh. bilioni 403.

Katika ufunguzi huo, Rais Magufuli alisema awamu ya pili ya mradi huo itahusisha barabara ya urefu wa kilometa 19.3 inayotoka Gerezani, eneo la Kariakoo hadi Mbagala Rangi Tatu, pamoja na ujenzi wa barabara ya juu katika makutano ya Barabara ya Nyerere na Kawawa.

Pia alisema awamu ya tatu itahusisha Barabara ya Nyerere hadi Gongo la Mboto yenye urefu wa Kilometa 33.6.Alisema awamu ya nne ni barabara yenye kilomita 25.9 ikihusisha Barabara ya Ali Hassan Mwinyi na Tegeta yenye urefu wa kilometa 22.8.

Rais alisema awamu ya tano ya mradi huo itahusisha barabara yenye urefu wa kilometa 27.9. Mradi huo unafadhiliwa na Benki ya Dunia (WB).

Awamu ya kwanza ya mradi wa ujenzi wa miundombinu ya BRT yenye urefu wa Km 20.9 unaojumuisha barabara ya Kimara–Kivukoni, Magomeni- Morocco na Fire–Kariakoo ulikamilika Desemba mwaka 2015 na huduma ya mabasi ilianza Mei 10, mwaka jana.

Mradi wa ujenzi wa miundombinu ya BRT una lengo la kupunguza msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam.
ads
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya SWAHILI NEWS kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Share To:

SWAHIBA MEDIA STAFF

Habari , karibu katika mtandao wetu ili kuhabarika na stori zote za siku katika lugha yetu adhwim ya kiswahili, habarika wakati wote weka dunia kiganjani mwako na swahili news

Post A Comment: