Balozi wa China nchini, Wang Ke amesema nchi hiyo itaendelea kuleta madaktari Tanzania ili watoe huduma za afya katika hospitali mbalimbali na kuwapa uzoefu wenzao.


Wang alisema hayo juzi wakati katika hafla ya kuwaaga madaktari 25 wa nchi hiyo waliokuwapo nchini kwa miaka miwili na kuongeza kuwa hadi sasa Watanzania 15.2 milioni wametibiwa na madaktari wa kujitolea wa China walioanza kuja Tanzania tangu mwaka 1968.

Alisema madaktari hao walioagwa walikuwa wakitoa huduma wakisaidiana na wenzao wa Tanzania wakiwamo wa hospitali za Muhimbili, Tabora, Musoma na Dodoma.

Balozi Wang alisema madaktari hao wamebobea katika magonjwa mbalimbali ukiwamo wa moyo.

“Mbali na kuhudumia hospitali hizo, walikwenda vijijini kuwafuata wagonjwa na kuwahudumia,” alisema na kuongeza kuwa katika awamu hiyo ya 24, madaktari hao wametoa dawa na vifaa tiba vyenye thamani ya Sh125 milioni.

Balozi Wang alisema baada ya madaktari hao kuondoka, watakuja wengine kwa kuwa mpango huo ni endelevu.

“Tutaendelea kuleta madaktari ili washirikiane na wenzao wa Tanzania,” alisema.

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alisema mpango wa Serikali ni kuhakikisha wagonjwa wote wanatibiwa nchini badala ya kuwapeleka nje ya nchi.

Alisema ili kufanikisha lengo hilo, Hospitali ya Taifa Muhimbili na hospitali za kanda zinahitaji kuboresha huduma zake.

Mwalimu alisema Serikali imeiomba China madaktari 11 watakaofanya kazi Muhimbili, Taasisi ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu Muhimbili (MOI), Hospitali ya Rufaa Mbeya na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI).

Kiongozi wa madaktari hao, Dk Sun Long alisema kwa miaka miwili waliyokaa Tanzania wamewapa uzoefu wenzao waliopo nchini.

Dk Sun ambaye ni daktari wa upasuaji wa moyo alisema madaktari wa moyo ni wachache Tanzania, hivyo ameshauri wasomeshwe wataalamu wa aina hiyo.
ads
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya SWAHILI NEWS kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Share To:

SWAHIBA MEDIA STAFF

Habari , karibu katika mtandao wetu ili kuhabarika na stori zote za siku katika lugha yetu adhwim ya kiswahili, habarika wakati wote weka dunia kiganjani mwako na swahili news

Post A Comment: