SHILINGI ya Tanzania imeendelea kuimarika kipindi chote mwaka huu ikiendelea kupanda na kushuka kwa shilingi 100 dhidi ya Dola ya Marekani kwa muda wa miezi 10 iliyopita.


Aidha taarifa ya Benki Kuu inaonesha kwamba taifa lina hazina ya kutosha ya fedha za kigeni na kutaka wananchi wasiwe na taharuki. Data za Benki Kuu zinaonesha shilingi ya Tanzania ilifungua mwaka ikiwa 2,186/21 lakini Ijumaa ilifunga kwa 2,247/78 , ikiwa imeshuka kwa asilimia 2.7. Pamoja na taarifa hiyo BoT imesema wananchi hawana sababu ya kuwa na taharuki.

“Benki Kuu inapenda kutoa taarifa kuwa hadi kufungwa kwa soko la jumla la kigeni linaloendeshwa na Benki Kuu leo jioni (Novemba 3) shilingi ya Tanzania inauzwa kati ya shilingi 2,246 na senti 50 na shilingi 2,247 na senti 60 kwa dola ya Marekani,“ ilisema taarifa hiyo. Hata hivyo, wachumi walibainisha kuwa kushuka kwa asilimia 2.7 hakuna maana kwenye uchumi, kwani athari yake ni kidogo sana kwenye uagizaji.

Katika ufafanuzi uliotolewa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kuhusu taarifa za awali za takwimu za Bloomberg kuonesha kushuka kwa shilingi hadi kufikia 2,481/83 kwa dola ya Marekani, ilisema kwamba kuna kasoro katika takwimu hizo na kwamba walishawaambia watu hao na wamefanyia mabadiliko. “Wakati Ijumaa soko la fedha za kigeni la Benki Kuu likifungwa, shilingi ya Tanzania ilikuwa inauzwa kati ya shilingi 2,246/50 na 2,247/60 kwa dola ya Marekani … Bloomberg inarekebisha tatizo hilo,” ilisema taarifa ya BoT iliyoitoa juzi jioni.

Kwa mujibu wa BoT, baada ya kuwasiliana na Bloomberg kuhusu suala hilo, walithibitisha kuwa baadhi ya wachangiaji waliingiza takwimu zisizo sahihi na hivyo marekebisho yameanza kufanyika. “Benki iliwasiliana na Bloomberg na walithibitisha kuwa kuna wachangiaji walioingiza takwimu zisizo sahihi na hivyo, walianza kufanya marekebisho,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo. Pamoja na masahihisho yaliyoelekezwa, Benki Kuu imesema kwamba kuna hazina ya kutosha ya fedha za kigeni na hakuna sababu ya taharuki.

Kampuni ya udalali ya soko la hisa Dar es Salaam pia juzi iliripoti kuwa wastani wa shilingi katika mauzo kwa mujibu wa BoT ilikuwa “2,237/33 na kununuliwa 2,226/20 na kuuzwa 2,248/46” dhidi ya dola ya Marekani. Hata hivyo, data za uchumi wa biashara zinaonesha shilingi ilifikia kiwango cha juu 2,260/80 mwezi Juni 2015. Miaka ya karibuni kiwango cha chini kilifikia 1,014/30 mwezi Desemba 2004.

Mchumi kiongozi wa Benki ya Maendeleo ya TIB, Dk Hildebrand Shayo alisema hata sarafu za mataifa makubwa duniani zimekuwa zikiyumbayumba baada ya fedha ya China Yuan kuingizwa kama fedha ya kimataifa. “Hili ni jambo la kimataifa kwa sasa, limesababishwa na kukubaliwa kwa yuan na sera mpya ya viwanda ya Marekani. Lakini hapa nyumbani, thamani ya kweli ya shilingi inaonekana, ikiambatana na sera ya sasa ya viwanda, kuongeza thamani ya malighafi yetu,” alisema Dk Shayo.

Mchumi huyo ambaye pia ni mtaalamu wa benki alisema athari ingehisiwa kama kiasi cha uuzaji nje kingekuwa kikubwa. “Athari itaonekana kidogo kwenye uingizaji bidhaa na hasa kwenye mafuta. Hii ndio bidhaa kubwa inayokula fedha zetu za kigeni,” alisema Dk Shayo na kuongeza kuwa vinginevyo athari ni ndogo sana.

Alhamisi, Benki ya CRDB ilisema msukumo dhidi ya shilingi unaendelea kupungua baada ya shilingi na dola kutofautiana kwa pointi za msingi kwa asilimia 68 ukilinganisha na awamu iliyopita kutokana na kusukumwa na mlinganisho wa viwango vya ugavi na mahitaji. Shinikizo dhidi ya sarafu ya ndani imeendelea kupungua.

“Kiwango cha mlinganisho wa mahitaji na usambazaji kimechangia kutulia, lakini mtiririko wa wadau wa korosho umeongeza kupunguza msukumo kwenye sarafu ya ndani,” ilisema CRDB katika ripoti yake ya Soko.

Benki nyingine, NMB ilitabiri shilingi kuendelea kuongezeka thamani dhidi ya dola ya Marekani siku zijazo. “Sisi NMB tunatarajia shilingi kuongezeka kesho kwani tunaelekea mapumziko ya mwisho wa wiki,” ilisema ripoti ya soko na benki hiyo iliongeza kuwa awamu ya pili ya biashara ya mwezi iliacha shilingi ikiongezeka thamani dhidi ya dola, ikitiwa msukumo na uingizaji mkubwa kutoka kwenye kilimo na taasisi.

Credit - Habarileo
ads
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya SWAHILI NEWS kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Share To:

SWAHIBA MEDIA STAFF

Habari , karibu katika mtandao wetu ili kuhabarika na stori zote za siku katika lugha yetu adhwim ya kiswahili, habarika wakati wote weka dunia kiganjani mwako na swahili news

Post A Comment: