OPERESHENI endelevu ya Shirika la Umeme nchini (Tanesco), inayofanywa mkoani hapa, imewanasa baadhi ya wateja wakiiba umeme kwa zaidi ya siku 1000 bila malipo halali.


Udanganyifu huo unaofanywa kwenye nyumba za biashara na makazi kwa kutumia mita za Luku, umebaini baadhi ya wateja kujiunganishia umeme moja kwa moja na wengine kwa kuchezea mita.

Ukaguzi wa jana ulihusisha maeneo ya Ngaramtoni, Oldadai, Soko la Kilombero, Makao Mapya, Mjini Kati na King’ori wilayani Arumeru.

Ofisa Usalama Mwandamizi kutoka makao makuu ya Tanesco, Dar es Salaam, Lenin Kiobya, akiongoza kikosi maalumu cha ukaguzi, alisema, wizi huo unadhoofisha juhudi za kuletea maendeleo kwa wananchi hususan, katika kipindi hiki cha Tanzania ya viwanda.

Kikosi hicho kinahusisha Idara za Mawasiliano, Udhibiti wa Mapato, Usalama na maofisa wa Arusha.

Alisema wizi huo unalipunguzia shirika ufanisi wa kuhudumia wananchi kwa kukwepa kulipa malipo halali.

Alisema baadhi ya wafanyakazi ambao siyo waaminifu wanakula njama na wateja kuiba umeme.

Alisema katika eneo la King’ori operesheni hiyo ilifanikiwa kubaini baadhi ya wateja waliojiunganishia umeme, huku wengine wakifanya udanganyifu kwenye mita za Luku.

Alisema baadhi ya mita zimefungwa juu ya nguzo za barabarani, lakini kwa kutumia watu wanaoitwa ‘vishoka’ wanafanikiwa kuzichezea na hivyo kukwepa kulipa malipo halali.

Alisema kwa kutumia mifumo yao, wanaweza kuwabaini kwamba hawajanunua umeme wa Luku kwa muda mrefu.

“Tumefanya ukaguzi na kuwanasa wateja waliokwepa kununua umeme wa Luku kwa siku hadi 1,000 huku wakiendelea kupata umeme,” alisema.

Alisema ukaguzi wao una lengo la kukusanya na kudhibiti upotevu wa mapato ya shirika.

Kwa upande wake, Mdhibiti Mapato Tanesco mkoani hapa, Mhandisi Hassan Juma, aliwataka wafanyakazi wa shirika kushirikiana kuhakikisha mafundi wasio waaminifu wanaondoka.
ads
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya SWAHILI NEWS kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Share To:

SWAHIBA MEDIA STAFF

Habari , karibu katika mtandao wetu ili kuhabarika na stori zote za siku katika lugha yetu adhwim ya kiswahili, habarika wakati wote weka dunia kiganjani mwako na swahili news

Post A Comment: