RAIS wa Ufilipino, Rodrigo Duterte amesema hana mchezo katika vita dhidi ya dawa za kulevya na hata ikibainika mwanaye ni mmoja wa wahusika, hakuna namna, ni kumuua tu.


Rais huyo ametoa maelezo hayo baada ya kuwapo kwa tuhuma zinazomhusisha mmoja wa wanawe ambaye anachunguzwa na polisi. Paolo Duterte kijana mwenye umri wa miaka 42, ambaye pia ni mwanasiasa mwezi huu aliitwa mbele ya baraza la uchunguzi kuhojiwa na alikana tuhuma dhidi yake. Kijana huyo alituhumiwa na mmoja wa wanasiasa kwamba ni sehemu ya genge la raia wa China, akihusika kusaidia genge hilo katika usafirishaji wa dawa za kulevya kutoka China.

Lakini katika mazungumzo yake ya hivi karibuni Duterte hakulenga moja kwa moja kuzungumzia kwa kina tukio hilo linalomhusu mwanawe huyo lakini akaweka wazi kwamba, hakuna mwanawe anayejihusisha na dawa za kulevya lakini hata hivyo, ikibainika anapaswa kuadhibiwa kama wengine.

“Niliwahi kusema na kwa kweli amri yangu ni kwamba: kama ninao watoto wanaojihusisha na dawa za kulevya, wauawe tu kama wahalifu wengine ili kuondoa minong’ono ya watu,” alisema Duterte katika hotuba yake mbele ya watumishi wa serikali aliokutana nao katika Ikulu ya Manila.

“Kwa hiyo nakwambia wewe Pulong (hilo ni jina la utani la Paolo mwanawe anayetuhumiwa kwa dawa za kulevya), amri yangu inaelekeza uuawe kama itathibitika. Na nitamlinda polisi atakayekuua, kama itakuwa ni kweli,” alisema

Duterte mwenye umri wa miaka 72 sasa amekuwa akiendesha kampeni kali dhidi ya biashara ya dawa za kulevya nchini mwake na alikwishaagiza yeyote atakayebainika kujihusisha na biashara hiyo auwawe, iwe mtumiaji au mfanyabiasara wa dawa hizo.

Tangu aingie madarakani katikati ya mwaka jana, 2016, polisi wamekwishaua watu zaidi ya 3,800 katika operesheni ya kupambana na dawa za kulevya katika taifa hilo.

Duterte alikaririwa akisema “ninayo furaha kuua” watu milioni hata tatu hivi walioathiriwa kwa matumizi ya dawa za kulevya, na kama kuna watoto waliouawa kwenye operesheni dhidi ya dawa za kulevya basi ni ajali ya bahati mbaya tu.

Tayari wasaidizi kadhaa wa Duterte wamekuwa wakiwaonya waandishi wa habari kwamba wasitilie maanani kila anachokisema kiongozi huyo.
ads
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya SWAHILI NEWS kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Share To:

SWAHIBA MEDIA STAFF

Habari , karibu katika mtandao wetu ili kuhabarika na stori zote za siku katika lugha yetu adhwim ya kiswahili, habarika wakati wote weka dunia kiganjani mwako na swahili news

Post A Comment: