STAFU Sajenti Nyangea (53), jana aliwasilisha mahakamani maelezo aliyoyanukuu kutoka kwa Josephine Mushumbusi kwamba alimtibu tiba mbadala marehemu Steven Kanumba (wakati wa uhai wake) na kwamba majibu ya vipimo hivyo yalibainisha kuwa ana maradhi ya moyo na mafuta mengi mwilini.


Kadhalika, Nyangea alinukuu maelezo kwamba majibu yalionyesha Kanumba alikuwa na maradhi ya upungufu wa hewa katika ubongo wake na kwamba maradhi yake yangeweza kusababisha mwili kupooza au kifo.

Mshitakiwa katika kesi hiyo ni Elizabeth Michael maarufu kama Lulu katika uigizaji wa filamu

Nyagea alinukuu maelezo hayo jana mbele ya Jaji Sam Rumanyika anayesikiliza kesi hiyo katika Mahakama Kuu Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam.

Awali kabla ya kuanza kuyanukuu maelezo hayo mahakamani, upande wa utetezi ukiongozwa na Wakili Peter Kibatala, uliiomba mahakama Stafu Sajenti Nyagea kuyawasilisha kama kilelezo maelezo aliyoandika kutoka kwa Mushumbus Aprili 23, 2012 wakati akiwa na cheo cha Sajenti.

Alidai kuwa anayatambua maelezo hayo kwa kuwa ndiye aliyeandika na mahakama ilikubali kuyapokea kama kielelezo.

Aidha, mahakama ilikubali kupokea maelezo na kumwamuru Nyagea kuyasoma kama alivyonukuu.

Alinukuu kwamba: “Daktari Josephine S. Mushumbusi (46) mkazi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Bunju, ni mmiliki wa kliniki ya Greshaz iliyopo Mawasiliano Tower natoa huduma ya tiba mbadala.

“Steven Kanumba alikuwa mteja wangu tangu Agosti, 2011 alipokuja kwa ajili ya kutoa sumu mwilini, tangu hapo alikua na mazoea ya kuja katika kliniki yangu kwa ajili ya huduma na alikuja mara kwa mara.

“Katika kupima, nilibaini kuwa ana matatizo ya mafuta mengi mwilini, maradhi ya moyo na upungufu wa hewa katika ubongo... matatizo hayo yalimletea udhaifu na alikuwa na maumivu ya moyo mara kwa mara na kuchoka mwili.

“Kanumba alikuwa anafanya mazoezi ya kutanua mwili, nilimshauri aachane nayo kwa kuwa yangemletea hatari ya kupooza mwili au kifo... mara nyingi misuli yake hubadilika rangi na kuwa ya bluu.

“Kwa sababu alifahamu kuwa natoa ushauri, alinieleza kwamba ana maumivu yanayoumiza sana moyo wake, lakini hakueleza matatizo gani, aliomba ushauri nasaha lakini kwa sababu nilikua na watu wengi tulipanga kukutana wakati mwingine, nikasikia amepoteza maisha.”

Baada ya kunukuu maelezo ya Mushumbus, Nyangea alimkabidhi mpelelezi wa kesi hiyo Erinatus.

Upande wa utetezi ulidai kuwa umefunga ushahidi wake na kwamba mtu anayeitwa na mahakama kwa ajili ya kutoa nyaraka, upande kinzani hauna mamlaka ya kumhoji.

Upande wa Jamhuri ulioongozwa na Mawakili wa Serikali, Faraja George, Yusuph Aboud na Batilda Mushi, ulidai kuwa hauna nia ya kumhoji ofisa huyo wa polisi kwa sababu maelezo hayo hayajui zaidi ya kuyanukuu.

Jaji alisema kesi hiyo itaendelea leo kwa ajili ya kuwasomea muhtasari wazee wa baraza ili waweze kutoa maoni ya majumuisho yao ya mwisho.

Alisema mshtakiwa ataendelea kuwa nje kwa dhamana.

Katika kesi ya msingi, ilidaiwa kuwa Aprili 7, 2012 Vatican Sinza, jijini, mshtakiwa alimuua bila kukusudia Kanumba. Mshtakiwa alipokumbushwa shtaka lake alikana.
ads
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya SWAHILI NEWS kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Share To:

SWAHIBA MEDIA STAFF

Habari , karibu katika mtandao wetu ili kuhabarika na stori zote za siku katika lugha yetu adhwim ya kiswahili, habarika wakati wote weka dunia kiganjani mwako na swahili news

Post A Comment: