WAKATI maafa zaidi yameripotiwa kusababishwa na mvua kubwa iliyonyesha jijini Dar es Salaam na mkoani Pwani, mvua kubwa nyingine inatarajiwa kunyesha leo na kesho katika maeneo mbalimbali ya Kanda ya Ziwa na Magharibi.


Hadi juzi watu watatu waliripotiwa kufariki dunia kutokana na mvua zinazoendelea jijini Dar es Salaam, huku nyumba 100 zikisombwa na maji na nyingine 700 kuzingirwa na maji hadi jana.

Aidha watu wengine wawili wamefariki dunia kufuatia mvua iliyonyesha juzi mkoani Pwani, ambapo miili yao imeweza kugundulika baada ya maji kupungua kwenye Mto Mpiji unaotenganisha mikoa ya Pwani na Dar es Salaam.

Mvua kubwa Kanda ya Ziwa leo

kesho Hata wakati bado machungu hayo hayajaisha; Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) imetangaza kuwa vipindi vya mvua kubwa, vinatarajiwa leo na kesho katika baadhi ya maeneo ya ukanda wa Ziwa Victoria na Magharibi ya nchi.

Taarifa ya Mamlaka hiyo iliyotolewa ilisema kuwa vipindi vya mvua kubwa inayozidi milimeta 50 ndani ya saa 24, vinatarajiwa katika baadhi ya maeneo ya ukanda wa Ziwa Victoria na Magharibi mwa nchi.

Ilisema kuwa baadhi ya maeneo ya mikoa ya Mara, Mwanza, Simiyu, Shinyanga, Geita, Kagera, Tabora, Katavi na Rukwa itakumbwa na mvua kubwa na kwamba hali hiyo inatokana na kuimarika kwa ukanda wa mvua katika maeneo hayo.

Maafa Dar es Salaam Katika tukio la Dar es Salaam, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa alisema Oktoba 26 mwaka huu eneo la Mwananyamala Kisiwani wilayani Kinondoni, Polisi walipokea taarifa ya kufa maji mwanamme mmoja ambaye hakufahamika jina lake mara moja mwenye umri unaokadiriwa kati ya miaka 30 na 35.

Alisema kifo hicho kilitokea baada ya kusombwa na maji ya Mto Ng’ombe, ambao ulifurika kutokana na mvua kubwa iliyokuwa inanyesha. Alisema tukio lingine la kifo lilitokea siku hiyo hiyo maeneo ya Tabata Kimanga wilayani Ilala, ambapo ulionekana mwili wa mtu jinsia ya kiume unaelea kwenye maji ndani ya Mto Tenge, baada ya askari kufuatilia waligundua kifo hicho kimetokana na mvua.

Alisema mwili huo haukutambulika kwa jina lake wala anakoishi, unakadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 20 hadi 22. Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Wakati huo huo, eneo la Kiluvya Kwa Komba mtoto aliyefahamika kwa jina la Teddy Narasco (8), ambaye ni mwanafunzi wa darasa la pili katika Shule ya Msingi Kiluvya alifariki dunia baada ya kusombwa na maji wakati akijaribu kujiokoa kutokana na maji mengi yaliyokuwa yamezingira nyumba yao.

Katika hatua nyingine, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi alisema, nyumba zaidi ya 100 zimebomoka na nyingine zaidi ya 700 bado zimezingirwa na maji katika maeneo mbalimbali ya wilaya ya Kinondoni hiyo kutokana na mafuriko ya mvua hiyo.

Aliyasema hayo alipokuwa akifanya ziara ya kukagua madhara, yaliyosababishwa na mvua hizo kwenye maeneo mbalimbali ya wilaya yake. Madhara mengine yaliyosababishwa na mvua hizo ni kuvunjika na kusombwa kwa daraja la Mto Mbezi eneo la Kwa Malecela Kawe, linalounganisha Mtaa wa Mzimuni na Mbezi Beach A.

Madaraja mengine yaliyoathirika kwa kuvunjika kingo zake ni daraja la Mbezi Juu Tangi Bovu na daraja la Mbweni, linaolounganisha Mtaa wa Ununio Kata ya Kunduchi na Mtaa wa Malindi Kata ya Mbweni.

Kwa mujibu wa Hapi, daraja la Mbweni lilijengwa na Serikali kupitia Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa gharama ya Sh milioni 700. Daraja hilo lilizinduliwa Mei 30, mwaka huu na Kiongozi wa Mbio za Mwenge, Amour Hamad Amour.
ads
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya SWAHILI NEWS kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Share To:

SWAHIBA MEDIA STAFF

Habari , karibu katika mtandao wetu ili kuhabarika na stori zote za siku katika lugha yetu adhwim ya kiswahili, habarika wakati wote weka dunia kiganjani mwako na swahili news

Post A Comment: