HATIMAYE jitihada za serikali kuwabana wakwepa kodi, wakiwamo waliokuwa wanapiga mabilioni ya shilingi kutokana na taarifa zisizo sahihi za uzalishaji madini na mauzo ya vituo vya mafuta,-


Zimezaa matunda baada ya jana Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kubainisha kuongezeka kwa makusanyo katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka huu wa bajeti.

Taarifa iliyowekwa jana kwenye tovuti rasmi ya TRA ilionyesha kuwa katika kipindi hicho cha miezi mitatu iliyopita, mamlaka hiyo ilikusanya Sh. trilioni 3.65, ikiwa ni ongezeko la asilimia 1.2 ikilinganishwa na makusanyo ya kipindi kama hicho kwa mwaka wa fedha 2016/17.

Taarifa hiyo ilifafanua kuwa makusanyo ya Julai yalikuwa Sh. trilioni 1.1, Agosti Sh. trilioni 1.2 na Septemba Sh. trilioni 1.3. Julai mwaka jana makusanyo ya TRA yalikuwa Sh. trilioni 1.07, Agosti Sh. trilioni 1.15 na Septemba Sh. trilioni 1.38.

Alipotafutwa na gazeti la  Nipashe kwa njia ya simu kuzungumzia sababu za kupaa kwa makusanyo hayo, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo, alisema mbali na mambo mengine, jitihada za serikali kupambana na ukwepaji kodi zimesaidia kwa kiasi kikubwa.

Katika miezi ya hivi karibuni, serikali ilitilia mkazo ukusanyaji wa mapato kwenye sekta ya madini kwa kuimarisha ufuatiliaji wa mfumo wa uchimbaji na biashara ya madini nchini.

Ni kutokana na jitihada hizo mwezi uliopita serikali ilifanikisha kukamata almasi ya mabilioni ya shilingi kwenye Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam ikiwa mbioni kusafirishwa kwenda ughaibuni huku ikibainika wahusika walikuwa wamedanganya uhalisia wa vipimo vyake kwa lengo la kukwepa kodi.

Katika ufafanuzi wake jana, Kayombo alisema sababu nyingine ya kupaa kwa makusanyo ya TRA ni kibano kwa wenye vituo vya mafuta ambao hivi karibuni walitakiwa kufunga mashine za kutoa stakabadhi za mauzo hayo na hamasa ya viongozi wa ngazi zote kusimamia ukusanyaji wa mapato.

SIKU 14
Julai 19 Rais John Magufuli aliamuru ndani ya siku 14 wamiliki wa vituo vyote vya mafuta nchini wamefunga na kuanza kutumia mashine za kielektroniki za kutolea risiti la sivyo wafutiwe leseni.

Rais Magufuli aliagiza Wizara ya Fedha na Mipango na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kuhakikisha vituo vyote vya mafuta nchini vinatumia mashine hizo na kusisitiza kuwa wamiliki watakaokiuka agizo hilo vituo vyao vifungwe na kufutiwa leseni.

"Na kwa hili natoa siku 14, wale wenye vituo vya mafuta wote, uwe upo Chato, uwe Biharamulo, uwe Kagera, uwe Dar es Salaam hakikisha una hiyo mashine ndani ya siku 14," alisema Rais Magufuli.

Rais Magufuli alitoa agizo hilo kuongeza nguvu baada ya TRA kuwa ilishaanza kuvifungia vituo vya mafuta kutokana na kutofunga mashine za kielektroniki kwenye pampu za mafuta.

Kayombo alisema siri nyingine ya kuongezeka kwa makusanyo yao ni mwamko wa Watanzania kulipa madeni yao ya kodi baada ya kuona fedha zinatumika kwenye shughuli za maendeleo zinazowanufaisha wote.

"Jingine ni serikali kurejesha nidhamu ya uwajibikaji na maadili kwa watendaji, watumishi waliohusika na ufisadi na rushwa wamechukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria," Kayombo alisema.

"Kwa sasa tumeziba mianya yote iliyotoa nafasi ya kuvuja kwa fedha za umma.

"Tunakusanya kila kilicho stahili ya serikali."

Kayombo aliwashukuru wananchi wanatoa taarifa zinazosaidia kukusanya mapato baada ya kuona fedha zao zinatumika vizuri.

Alisema makusanyo hayo yamejumuisha vyanzo vingi vya mapato ikiwamo maeneo ya madini, biashara na kodi za majengo huku akiwataka wafanyabiashara wa michezo ya kubahatisha kulipa kodi zao kwa mujibu wa Sheria ya Michezo ya Kubahatisha Sura Namba 41.
ads
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya SWAHILI NEWS kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Share To:

SWAHIBA MEDIA STAFF

Habari , karibu katika mtandao wetu ili kuhabarika na stori zote za siku katika lugha yetu adhwim ya kiswahili, habarika wakati wote weka dunia kiganjani mwako na swahili news

Post A Comment: