Pengine ni katika harakati za kuutafuta utanashati au ukosefu wa ajira, na huenda ikawa ni mtindo wa kimaisha kwa vijana wengi hapa nchini na duniani kote wanaotunisha misuli. Hata hivyo wanaume walio katika harakati za kutunisha misuli au kupata maumbo yenye miraba minne, wamekuwa wakitumia dawa ili kuyapata maumbo hayo badala ya kufanya mazoezi ya viungo.
Vijana wengi hivi sasa wananunua kwa wingi dawa za kutunisha misuli maarufu kama ‘doping’ kwa sababu zinazotajwa kuwa ni kutafuta ajira kama vile ulinzi kwenye kumbi za starehe, ulinzi wa watu maarufu(bodyguard) na wengine mashindano ya kunyanyua vitu vizito huku wengine wakiutafuta utanashati.
Steroids
Wataalamu wa afya wanataja baadhi ya dawa zinazonunuliwa na wajenga misuli kuwa ni Anabolic Steroids, ambazo husaidia kujaza misuli na kutochoka haraka.
Ripoti ya Wizara ya Afya na Huduma za Jamii ya Marekani inaeleza hivi: “Dawa za steroids za kuongeza ukubwa wa misuli ni kemikali zinazohusiana na homoni za kiume (tetosterones). Dawa hizo huchochea ukuzi wa misuli na kustawi kwa maumbile ya kiume. Wavulana wanapobalehe homoni hizo huongezeka na kubadilika na hivyo kuchochea mabadiliko ambayo humfanya mvulana awe mwanamume. Nyingine ni Creatine ambazo huuzwa katika hali ya unga unga na kama ilivyo Steroids, dawa hii nayo hujenga misuli na kuondoa maumivu ya mwili na Human Growth Hormone, vichocheo ambavyo hukuza misuli ya mtu kwa wiki chache tu.
Dawa nyingine zenye nguvu na zinazotumiwa zaidi na wanaume wanaotaka kujenga misuli ni Optimal Stack, Precision Power, Estoforce Edge, Muscle Ex Edge na Muscle Rip Edge.
Miaka ya 70, watunisha misuli wengi akiwemo Arnold Schwazenerger, walikiri kutumia Steroids kama dawa zinazowasaidia kukuza misuli yao hata hivyo mwaka 1990, Marekani, ilianzisha sheria ya kuzuia dawa za Steroids na kuiweka katika kundi la dawa zilizopigwa marufuku.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa baadhi ya vijana hutumia dawa za vichocheo vya wanaume kama testosterone kukuza misuli hiyo. Wengi hutumia dawa hizo kwa kiwango kikubwa kiasi cha mara 10 hadi 100 zaidi ya kile ambacho daktari anaweza kukuandikia.
Wengi huzipata dawa hizi nchini Afrika Kusini ambako huletwa na watu binafsi na kuzisambaza katika nyumba za mazoezi (gym) ambako vijana wengi hufanya mazoezi ya kujenga vifua.
Gosbert Msuya, mlinda mlango wa klabu ya muziki ya Maisha, anakataa kutumia dawa za kutunisha misuli, lakini anakubali kuwa wapo vijana wanaotumia dawa hizo kwa sababu mbalimbali kubwa ikiwa ni ajira na mwonekano. “Sasa ukiwa na mwili mkubwa unapata kazi za kuwalinda watu maarufu, kulinda ‘stage’ pindi wanamuziki wanapoburudisha. Ajira nyingine ni wakati wa maadhimisho makubwa ya kitaifa, kucheza filamu, na mwonekano mzuri,” anasema Msuya.
Kijana anayekunywa dawa hizi huweza kuongezeka kilo tano hadi 15 ndani ya miezi miwili. Mzunguko na msukumo wa damu yake huongezeka kiasi cha asilimia 20, jambo linalosababisha misuli yake kujaa.
Misuli hii huonekana wazi zaidi kwani dawa hizi husaidia kuchoma kalori kwa kiasi kikubwa n husababisha mwili kupoteza mafuta mengi.
Madhara
Madhara yanayoweza kuwakuta vijana wanaotunisha misuli kwa kutumia vidonge vya vichocheo au steroids ni pamoja na maradhi ya moyo, lehemu mbaya mwilini, chunusi, upara, mabadiliko ya utendaji kazi wa moyo, ini na figo huweza kuharibika. Wengine huweza kupata matiti kama ya mwanamke. Kwa upande mwingine, wanawake wanaotumia dawa hizi hupata sauti za kiume na ndevu. Mengine ni kukosa uwezo wa tendo la ndoa, kusinyaa au kupotea kwa korodani, tezi dume kukua, kuwa na hasira, shinikizo la damu.
Madhara mengine ni ogani muhimu kushindwa kufanya kazi ghafla, kama vile ini. Kifo cha ghafla, saratani na figo kushindwa kufanya kazi. Lakini pia, wataalamu wanasema wengi wanaotumia dawa hizi hugeuka kuwa wajeuri na wenye hasira za haraka.
Namna ya kumfahamu anayetunisha misuli kwa dawa
Ingawa ni vigumu kumfahamu mtu anayetumia dawa za kutunisha misuli kwa asilimia 100 hasa kwa wale ambao hawajatumia dawa kwa muda mrefu, lakini unaweza kumfahamu mtu aliyetumia dawa hizo.
Kwanza wengi hupata misuli mingi kwa wiki chache, na misuli yao hujitokeza nje ya ngozi kama imepigwa ‘pampu’.
Hata hivyo wataalamu wa afya wanasema, misuli ya mtu anayetumia dawa si imara kama ya mtu anayefanya mazoezi.
Watunisha misuli waliopatwa na vifo vya ghafla
Inasadikiwa kuwa asilimia kubwa ya watunisha misuli hawa, walifariki dunia ghafla kutokana na dawa za kutunisha misuli na wakati mwingine wakizichanganya na dawa za kulevya. Wa kwanza ni Carlos Rodrigues, Mohammed Benaziza, Chuck Sipes, Ray McNeil, Andreas Munzerm, Sonny Schimidt, Don Youngblood na Paul Demayo.
Mfamasia katika Hospitali ya Mirrs ya Mwenge, David Cyprian anasema, kikubwa kinachofanywa na watunisha misuli ni matumizi mabaya(abuse), ambapo dawa zinazotumika kufanya kitu kingine hutumiwa kujenga misuli. Anatoa mfano kuwa, dawa za vichocheo vya kiume(testosterone) na Steroids, zina kazi ya kuwasaidia watu wanaochelewa kupata balehe, wenye matatizo ya ugumba na waliopoteza uzito mkubwa kwa sababu ya maradhi ya HIV.
“Hata wanariadha nao hutumia dawa za aina hii kwa sababu ya kuongeza nguvu na kujenga misuli. Lakini ili kupata uhakika iwapo mtu ametumia dawa za aina hiyo, mkojo wake hupimwa” anasema.
Mlinzi Mkuu wa Ukumbi wa Swispub, Tabata na mwalimu wa mazoezi, Selemani Bwagege anashauri vijana kufanya mazoezi na kufuata nidhamu ya mazoezi badala ya kutumia dawa.
“Mambo mengine tunayaiga ingawa hayana umuhimu kwetu kiafya. Ukifanya mazoezi unapata umbile kubwa na langu,” anasema.
Anakiri kuwa, vijana wengi wanaotaka miili mikubwa wanafanya hivyo kwa ajili ya ajira.
Zifahamu dawa za Steroidi
Mfamasia wa Msuya anaeleza kuwa Steroidi zilitengenezwa viwandani kwa mara ya kwanza katika miaka ya 30 ili kuwatibu wanaume ambao walishindwa kutokeza homoni za kutosha. Leo, steroidi hutumiwa kurekebisha kudhoofika kwa mwili kunakosababishwa na virusi vya Ukimwi na magonjwa mengine.
“Hata hivyo, Steroidi hutumiwa sana na watu wasio na uhitaji wa kitiba. Katika miaka ya 50, steroidi zilianza kupatikana kimagendo, na wana-michezo waliojitakia sifa walianza kuzitumia kuongeza nguvu mwilini,” anasema.
TFDA wazungumzia dawa hizo
Msemaji wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Gaudensia Simwanza anasema dawa za kutunisha misuli zinaingia nchini kwa utaratibu wa uingizaji wa dawa na kabla ya kusajiliwa hupitia maabara na kupimwa.
Hata hivyo, anasema dawa hizo zinapotumika bila kuandikiwa na daktari na kutumiwa kiholela, huweza kusababisha madhara ingawa zikitumika kwa sababu husika madhara ni madogo, lakini zikitumiwa kwa sababu nyingine husababisha madhara.
Post A Comment: