Fungamano la Makanisa ya Kilutheri Duniani (LWF) limekutana nchini kujadili namna ya kutetea watu waliotengwa wakiwemo wenye ulemavu.


Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Alex Malasusa ambaye ndiye mwenyeji wa ugeni huo amesema ipo haja ya kanisa kupaza sauti kuwatetea watu hao, wakiwemo wenye ulemavu, wanawake na watoto.

Dk Malasusa amesema kanisa lina wajibu wa kuona haki inatendeka kwa watu wote bila kubaguliwa hali zao na uwezo wao katika kufanya mambo.

Kuhusu sera zilizopo, Dk Malasusa amesema ifike wakati Serikali ianze kuziangalia kwa jicho la tatu ili kuhakikisha hakuna anayeachwa nyuma.

“Tumeona kuna kundi ambalo limeachwa nyuma kwa muda mrefu, mfano walemavu. Katika nchi nyingi za Kiafrika walemavu wamekuwa wakionekana kama laana, wanafungiwa ndani,” amesema.

Dk Malasusa amesema, “Katika nchi nyingi utamaduni wa watu ndiyo unawezesha utengenezaji wa sera, hivyo ifike wakati zitengenezwe sera ambazo zitawafanya watu wote wapate haki zao inavyostahili bila kujali ni mlemavu, mwanamke au mtoto.”

Akifungua kongamano hilo. Rais wa LWF na Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Nigeria, Musa Filibus amesema haitoshi kwa kanisa kuilaumu au kuinyooshea kidole Serikali wakati lenyewe halijatimiza wajibu wake katika kukabiliana na changamoto zilizopo kwenye jamii.

Amesema wajibu huo unaanza kuonekana kwa kuonyesha njia mbadala za kukabiliana na changamoto hizo, ikiwa ni pamoja na kukemea vitendo visivyofaa.

“Tukiwaelimisha watoto wa kike tutapunguza mimba na ndoa za utotoni, vifo vinavyotokana na watoto kujifungua wakiwa na umri mdogo na mambo mengine kama hayo,” amesema.

Mshiriki wa kongamano hilo, Dk Hellen Kijo- Bisimba amesema ipo haja kwa kanisa  kupambana na mifumo inayosababisha walemavu, wanawake na watoto kuendelea kuwa kwenye kundi maalumu.

“Kanisa limekuwa likiwasaidia kwa kuwapatia vyakula, mavazi, malazi na hata elimu watu wenye mahitaji maalumu lakini bado lilikuwa halijajielekeza kupambana na mifumo inayowasababishia hali hiyo. Tumeanza kugeukia huko na tunataka kukabiliana nayo ili tuwe na nguvu ya kupaza sauti kwa ngazi za juu zaidi,” amesema Dk Kijo –Bisimba.
ads
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya SWAHILI NEWS kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Share To:

SWAHIBA MEDIA STAFF

Habari , karibu katika mtandao wetu ili kuhabarika na stori zote za siku katika lugha yetu adhwim ya kiswahili, habarika wakati wote weka dunia kiganjani mwako na swahili news

Post A Comment: