ads

UPANDE wa Jamhuri katika kesi inayomkabili Harbinder Singh Sethi umeiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, kuruhusu atibiwe katika Hospitali za Amana na Lugalo.


Aidha, Jamhuri imedai unafahamu kuwapo kwa amri ya mahakama hiyo ya kutaka Sethi akatibiwe Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, lakini hakuna ushahidi unaothibitisha kwamba Hospitali ya Amana imeshindwa kutoa matibabu ya maradhi ya mshtakiwa huyo.

Hoja hiyo ilitolewa jana na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Leonard Swai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi, baada ya wakili wa utetezi Alex Balomi kudai mteja wake hajapata matibabu licha ya mahakama hiyo kutoa amri mshtakiwa akatibiwe.

"Mheshimiwa hakimu tunakiri kwamba kuna amri ya mahakama mshtakiwa kwenda kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Muhimbili... lakini hatuna uthibitisho kuwa siku mshtakiwa alipokamatwa alikuwa anakwenda Afrika Kusini kutibiwa au la," alidai Swai.

Pia alisema si sahihi kwa mshtakiwa kupelekwa nje ya nchi kutibiwa kwa sababu utaratibu wa mgonjwa kupelekwa nje unafahamika, na kwamba haendi kwa sababu ya amri ya Mahakama.

Swai alipinga Sethi kutibiwa nje ya nchi kwa kuwa madaktari wa hapa nchini hawajatoa maelezo kwamba wameshindwa kumtibu maradhi yake.

"Mheshimiwa hakimu, hakuna utaratibu wa mgonjwa kupelekwa moja kwa moja Hospitali ya Muhimbili bila kuwa na rufani kutoka Hospitali ya Amana ama Lugalo," alisema Swai.

"Wao ndiyo watafanya utaratibu wa kumuhamishia (Muhimbili) ikiwa watashindwa kumpatia huduma stahiki."

Pia Swai alidai kuwa mahabusu aliko mshtakiwa anatibiwa, na kwamba magereza wanatakiwa kuthibitisha na kufanya utaratibu apelekwe Hospitali ya Amana.

Akifafanua hoja yake, Swai alidai kuwa upande wa Jamhuri unaomba mshtakiwa aendelee kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Amana hadi pale madaktari watakapothibitisha kuwa wameshindwa ndipo watampa rufani kwenda Muhimbili.

Aidha aliomba mahakama kupanga kutajwa kesi hiyo ndani ya siku 14 badala ya siku saba kama utetezi walivyoomba kwa kuwa watakua wanamsumbua mgonjwa na kwamba muda huo autumie kwenda hospitali na siyo mahakamani.

Hata hivyo, Juni 28, mwaka huu Hakimu Shaidi alitoa amri ya mshtakiwa kwenda kutibiwa hospitali ya Muhimbili na si nje ya nchi.

Hakimu alisema mahakama yake inatoa siku 14 kama upande wa Jamhuri ulivyoomba ili kuangalia kama atakuwa amefikishwa katika Hospitali ya Amana au Lugalo kupatiwa matibabu na kesi hiyo itatajwa Agosti 17, mwaka huu.

Mbali na Sethi, mshtakiwa mwingine ni James Rugemalira ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa VIP Engineering na mmiliki mwenza wa zamani wa kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Ltd (IPTL).

Wote wawili wanakabiliwa na mashtaka 12 ya uhujumu uchumi kwa kuisababishia serikali hasara ya dola za Marekani milioni 22.1 na Sh. bilioni 309 pamoja na utakatishaji fedha.

Wafanyabiashara hao waliposomewa mashtaka yao kwa mara ya kwanza mahakamani upande wa Jamhuri ulidai wanakabiliwa na mashtaka ya kula njama, kujihusisha na mtandao wa uhalifu, kughushi, kuwasilisha nyaraka za kughushi, kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu, kuisababishia serikali hasara na kutakatisha fedha.

Ilidaiwa kuwa kati ya Oktoba 18, 2011 na Machi 19, 2014 jijini Dar es Salaam walikula njama katika nchi za Afrika Kusini, Kenya na India ili kutenda kosa.

Aidha, ilidaiwa katika shtaka la pili kati ya Oktoba 8,2011 na Machi 19,2014 jijini Dar es Salaam wakiwa siyo watumishi wa umma walishirikiana na watumishi wa umma kutekeleza mtandao huo wa uhalifu kwa lengo la kujipatia faida.

Katika shtaka la tatu linalomkabili Sethi, inadaiwa kuwa Oktoba 10, 2011 katika Mtaa wa Ohio, Ilala Dar es Salaam akiwa na nia ya ulaghai alighushi fomu namba 14 A ya usajili wa kampuni na kuonyesha kuwa yeye ni Mtanzania anayeishi kitalu namba 887, Mtaa wa Mrikau, Masaki wakati akijua sio kweli.

Pia, Sethi anadaiwa alitoa nyaraka ya kughushi ambayo ni fomu namba 14 A ya usajili wa kampuni kwa Ofisa msajili wa Kampuni, Seka Kasera kwa nia ya kuonyesha kwamba yeye ni Mtanzania na mkazi wa Mtaa wa Mrikau, Masaki, Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Aidha, Kimaro alidai katika mashtaka ya kujipatia fedha kwamba kati ya Novemba 28 na 29, 2011 na Januari 23, 2014 katika makao makuu ya Benki ya Stanbic Kinondoni na Benki ya Mkombozi tawi la Mtakatifu Joseph, kwa ulaghai washtakiwa hao walijipatia kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BOT), dola za Marekani 22,198,544.60 na Sh. 309,461,300,158.27.

Pia washtakiwa wote wanadaiwa kuisababishia serikali hasara ambapo inadaiwa walitenda makosa hayo Novemba 29, 2013 katika Benki ya Stanbic tawi la kati, Kinondoni, na kwa vitendo vyao hivyo waliisababishia serikali hasara ya dola za Marekani 22,198,544.60 na Sh. 309,461,300,158.27.

Kimaro alidai kati ya Novemba 29, 2013 na Januari 23, 2014 katika maeneo tofauti Dar es Salaam, kwa pamoja walitenda kosa la kutakatisha fedha kwa kuchukua fedha kutoka BoT ambazo ni dola za Marekani milioni 22.1 na Sh. bilioni 309.4 wakati wakijua fedha hizo ni zao la kujihusisha na genge la uhalifu.

Katika shtaka la nane, Kimaro alidai kuwa Novemba 29, 2013 katika tawi la kati la Benki ya Stanbic Tanzania wilaya ya Kinondoni, Sethi alitakatisha fedha kwa kuchukua kutoka BOT, dola za Marekani milioni 22.1 wakati akijua fedha hizo zimetokana na zao la kujihusisha na genge la uhalifu.

Aidha, Sethi anadaiwa kuwa kati ya Novemba 29, 2013 na Machi 14,2014 katika tawi la kati la Benki ya Stanbic Kinondoni Dar es Salaam alitakatisha fedha, Sh. bilioni 309.4 kutoka BOT wakati akijua fedha hizo zimetokana na zao la uhalifu.

Katika shtaka la 10, inadaiwa kuwa Januari 23, 2014 katika Benki ya Mkombozi tawi la St Joseph Cathedral, Rugemalira alitakatisha fedha ambazo ni Sh. bilioni 73.5 kutoka kwa Sethi wakati akijua fedha hizo zimetokana na zao la kujihusisha na genge la uhalifu.

Pia ilidaiwa kuwa Januari 23, 2014 katika Benki ya Mkombozi tawi hilo, Rugemalira alitakatisha fedha ambazo ni dola za Marekani 22,000,000 kutoka kwa Sethi wakati akijua fedha hizo ni zao la uhalifu.

Pia Sethi anadaiwa kuwa Januari 28, 2014 katika tawi la kati la Benki ya Stanbic wilaya ya Kinondoni alihamisha kwenda Afrika

Kusini Rand 1,305,800 kwenda kwenye akaunti namba 022655123 katika Benki ya Standard Land Rover Sandton ya Afrika Kusini wakati akijua katika kipindi anahamisha, fedha hizo zimetokana na zao la kujihusisha na genge la uhalifu.

Washtakiwa hao hawakutakiwa kujibu chochote kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi.

Upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika na washtakiwa wamewekwa rumande kwa kuwa mashtaka ya kutakatisha fedha yanayowakabili hayana dhamana.
ads
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya SWAHILI NEWS kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Share To:

SWAHIBA MEDIA STAFF

Habari , karibu katika mtandao wetu ili kuhabarika na stori zote za siku katika lugha yetu adhwim ya kiswahili, habarika wakati wote weka dunia kiganjani mwako na swahili news

Post A Comment: