KOCHA Mkuu wa Yanga Mzambia, George Lwandamina amemaliza mazoezi ya fitinesi na jana jioni alitarajia kupanga vikosi viwili vitakavyocheza mechi mazoezi kwa ajili ya kuwaangalia wachezaji waliokuwepo kwenye majaribio. Wachezaji waliokuwepo kwenye majaribio ni kiungo Mcameroon,
Fernando Bongyang na beki wa kati Mnigeria, Henry Tonny Okoh anayemudu kucheza namba 4 na 5. Nyota hao, wamefikisha wiki nne tangu wamejiunga kwenye majaribio ya timu hiyo waliyoanza jijini Dar es Salaam kabla ya kwenda Morogoro kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu Bara.
Akizungumza na gazeti la Championi Jumatano, Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh alisema timu hiyo itacheza mechi hizo baada ya kumaliza programu ya mazoezi ya
fitinesi kwa muda wa siku mbili mfululizo wakicheza kwa dakika 90. Saleh alisema, Lwandamina atapanga vikosi viwili vya ushindani huku akiitumia ‘mechi’ hiyo kama sehemu ya kuangalia uwezo wa wachezaji hao kabla ya kuamua yupi anastahili kupewa mkataba. Aliongeza kuwa, kocha huyo pia atatumia mechi hiyo kwa ajili ya kuwaangalia wachezaji wapya waliowasajili hivi karibuni akiwemo Ibrahim Ajibu, Pius Buswita,
Rostand Youthe, Abdallah Shaibu ‘Ninja’ na Burhani Akilimali. “Leo (jana) asubuhi tumemaliza program ya mazoezi ya fitinesi, wachezaji walikuwa wanafanya mazoezi magumu ya kukimbia mbio ndefu na fupi kwa maparachuti na lengo ni kukiimarisha kikosi chetu.
“Jioni (jana) tunatarajia
kuanza mazoezi ya kuchezea mpira kwa wachezaji wetu baada ya kuona mazoezi yamewaingia na kikubwa kocha ataanza kwa kupanga vikosi viwili vyenye ushindani na kikubwa kumuangalia huyu kiungo Mcameroon na beki Mnigeria kabla ya kuamua yupi anayestaili kupewa mkataba Jangwani.
“Pia kocha ataitumia mechi hiyo ya mazoezi kwa ajili ya kuangalia uwezo wa kila mchezaji mpya aliyesajili, mechi hizo tutacheza kwa siku mbili mfululizo kwa dakika 90 kabla ya Jumamosi kurejea Dar,” alisema Saleh.
Post A Comment: