MAHAKAMA Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, imepanga kutoa kesho uamuzi wa kusikiliza ama kutosikiliza maombi ya wabunge nane wa CUF waliofukuzwa kwenye chama hicho na upande wa Profesa Ibrahim Lipumba.
Jana mahakama hiyo iliyoketi chini ya Jaji Lugano Mwandambo, ilipokea pingamizi la awali la upande wa walalamikiwa lililowasilishwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Gabriel Malata.
Upande wa walalamikiwa uliwasilisha pingamizi hilo wakipinga kufunguliwa kesi hiyo na jana majira ya saa 5:15 asubuhi mahakama hiyo ilianza shughuli zake hadi saa 9:15 alasiri.
Malata alidai kuwa anapinga kufunguliwa kesi hiyo kwa kuwa haina mashiko kisheria na kwamba haijafunguliwa kwa njia sahihi.
“Mtukufu Jaji, maombi haya yamefunguliwa bila kutumika kifungu sahihi kinachoipa mahakama hii mamlaka ya kusikiliza na kutoa uamuzi dhidi ya maombi yao,” alidai na kusema zaidi:
“Walalamikaji wamefungua maombi haya chini ya kifungu cha 2 kidogo cha (3) ambacho kinaipa mamlaka Mahakama kutumia sheria ya Jumuiya ya Madola… Kama yameletwa chini ya kifungu hicho ilipaswa kiwepo kifungu husika kutoka katika sheria ya Jumuiya ya Madola, kisheria kinapaswa kutumika endapo hakutakuwa na sheria yoyote Tanzania inayozungumzia maombi hayo."
Pia, alidai kuwa maombi hayo ni batili, hivyo yatupiliwe mbali kwa kuwa hata Mahakama iliwahi kutoa uamuzi dhidi ya kifungu hicho kilichotumika kufungulia.
Hoja nyingine, alidai Malata, ni kuwapo kwa hoja ndani ya maombi hayo kwamba kuna rufani ambayo imekatwa ndani ya chama na bado haijasikilizwa, kwa msingi huo itaichanganya mahakama.
Kadhalika, alidai kuwa maombi hayo yanaichanganya mahakama kwa sababu upande huo umefungua kesi mbili kwa wakati mmoja, ikiwamo rufani iliyokatwa ndani ya chama na kesi waliyofungua mahakamani namba 143/2017 huku wakijua si utaratibu mzuri wa kisheria, na mahakama haiwezi kutoa uamuzi katika kesi mbili zilizo kwenye mamlaka tofauti.
“Katiba ya Tanzania ibara ya 66(1), inatambua uwepo wa aina tatu ya wabunge ambao wanachaguliwa, viti maalum na wanaoteuliwa, kifungu cha 86(A) cha sheria ya Uchaguzi kinawaelezea wabunge wa viti maalum," alidai wakili huyo.
Alidai kuwa maombi yaliyofunguliwa yanataka kuzuiwa kwa wabunge wapya kuapishwa, lakini jukumu hilo si la mahakama bali ni mhimili wa Bunge chini ya Ibara ya 68.
Alidai hatua hiyo itakuwa ni uingiliaji wa majukumu kikatiba kwa sababu walalamikiwa wanaiomba mahakama kufanya shughuli za Bunge, wakati kisheria hairuhusiwi.
Alidai kuwa kutokana na hatua hiyo, hilo sio jukumu la Mahakama, kwani ikiachwa inaweza ikawa ndiyo tabia kwa wabunge kuwekewa pingamizi kila wanapochaguliwa.
Malata alidai kuwa endapo maombi hayo yataridhiwa na mahakama ama hayataridhiwa kuwa na gharama kwa waleta maombi.
Akijibu hoja hizo, wakili wa waombaji, Peter Kibatala alidai kuwa pingamizi la walalamikiwa halina mashiko kwa sababu ni msimamo wa kisheria kwamba inataka uweke zuio ikiwa kesi imeanza.
Aliomba mahakama hiyo itupilie mbali pingamizi hilo kwa sababu halina mashiko ya kisheria.
Kuhusu kifungu kilichotumika, alidai kuwa mahakama ilishawahi kufanya maamuzi mawili tofauti kwa kuwa alipokea kifungu hicho kama ilivyo.
“Mtukufu Jaji, hiyo Sheria ni ya Tanzania na ilirithiwa tu na Jumuiya ya Madola, kwani sheria hiyo ipo kila Jumuiya na hakuna haja ya kuwepo kwa kifungu, hivyo tunaomba pingamizi litupiliwe mbali,” alidai Kibatala.
Kibatala alidai kuwa Ibara ya 107 katika katiba ya Jamhuri ya Muungano inatamka kuwa Mahakama Kuu ndicho chombo cha mwisho cha utoaji haki.
Alidai kuwa wabunge hao wamekosa haki ya kusikilizwa katika chama na ndiyo sababu wameleta maombi ya kuzuia shughuli zisiendelee ikiwa ni pamoja na kutowaapisha wabunge wapya walioteuliwa.
Aliendelea kudai kuwa amewasilisha mahakamani hapo maombi saba na si lazima yajibiwe yote.
Baada ya mabishano ya kisheria, Jaji Mwandapo alisema baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, mahakama yake itatoa uamuzi Agosti 4 na kesi ya msingi itaanza kusikilizwa Agosti 31.
Post A Comment: