SERIKALI imezikataa zaidi ya Sh. milioni 40 zilizoingizwa kwenye akaunti ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Julai 10, mwaka huu, na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja.
Ngeleja ni mmoja wa watu waliopokea mgawo wa fedha zinazodaiwa kuwa zao la kashfa ya Tegeta Escrow lakini akatangaza kuzirejesha kwa TRA Jumatatu iliyopita.
Msemaji wa Wizara ya Fedha na Mipango, Benny Mwaipaja, aliliambia gazeti hili jana kuwa hadi sasa serikali haijajua misingi ya urejeshwaji wa fedha hizo kwa kuwa hakuna tamko au maelekezo ya kurejeshwa.
“Hatujui aliyemwambia arejeshe ni Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) au nani, hatujui ni msingi gani umetumika," alisema Mwaipaja na kueleza zaidi, "ninachojua suala la fedha za Escrow liko mahakamani ambayo itatoa uamuzi kwa mujibu wa Sheria."
"Aliyerejesha (Ngeleja) hatujui amesimamia misingi gani.”
Kwa mujibu wa Mwaipaja, serikali haijatoa tamko lolote la kutaka watu warejeshe fedha hizo kwa kuwa wahusika wako mahakamani, hivyo ni vigumu kwa Wizara yake kujua zinastahili kurejeshwa wapi kwa sasa.
Alisema kama fedha zimepelekwa TRA waulizwe wao kwani nayo ni taasisi ya serikali hivyo inaweza kuwa inajua imezipokea kwa misingi ipi.
Hata hivyo, Mkurugenzi wa Elimu kwa Umma wa TRA, Richard Kayombo aliiambia Nipashe kuwa mamlaka hiyo inahusika na kuhakikisha serikali inakusanya kodi stahiki na siyo urejeshaji wa fedha za kashfa kama Escrow.
Kayombo alitoa ufafanuzi huo wakati alipoulizwa na Nipashe juu ya utaratibu rasmi uliopo wa urejeshaji wa fedha hizo endapo wanufaika zaidi watataka kufuata nyayo za Ngeleja.
Akifafanua zaidi juu ya suala hilo, Kayombo alisema TRA haihusiki na fedha zilizochotwa kwenye akaunti ya Tegeta Escrow kwa kuwa hazikuwa mali yake.
Aidha, Kayombo alisema TRA haiwezi kuzizungumzia fedha hizo kwa kuwa hazijawahi kuwa mali yake na kuelekeza watafutwe wenye fedha hizo kwa ufafanuzi zaidi.
"Fedha za Escrow zinaihusu vipi TRA? Tunawezaje kukaa na kuzungumzia fedha ambazo si zetu?" Alisema Kayombo. "Mimi nashauri watafutwe wenyewe wazungumze... siyo sisi."
Aidha, chanzo cha kuaminika kutoka Benki Kuu (BoT) kiliiambia Nipashe jana kuwa “hakuna mahali ambapo BoT inaingia kwenye fedha za Escrow.”
Nipashe ilitaka kujua hatima ya fedha hizo kwa benki ya Serikali BOT, baada ya TRA kuzikana.
“BoT kuna akaunti za serikali, wenye akaunti ndiyo wanaweza kuzizungumzia na siyo sisi, watafuteni serikali wasema juu ya jambo hili,” kilisema zaidi chanzo hicho.
Ndipo Msemaji wa Wizara ya Fedha na Mipango aliposema hazitambuliki uwepo wake Serikalini.
UCHUNGUZI UNAENDELEA
Akizungumzia sakata hilo, Meneja Mawasiliano wa Takukuru, Musa Misalaba alisema hawajatoa maelekezo ya fedha hizo kurejeshwa na kwamba uchunguzi unaendelea kwa suala hilo.
“Kosa la jinai haliishi hadi mhusika afariki kama kuna kikwazo ni suala la muda, uchunguzi ni mchakato mrefu, kesi ya jinai inakuwapo inachukua muda mrefu. Tunaendelea nayo hadi ushahidi wa kuturidhisha kuwafikisha mahakamani ukamilike,” alisema.
Wiki iliyopita, Meneja huyo alieleza Nipashe kuwa hakuna yeyote aliyejihusisha na jinai atakayebakia salama kwa sasa, na kwamba kitakachotofautisha ni muda wa kila mmoja kufikiwa na mkono wa sheria.
Februari 2014, Ngeleja ambaye kwa sasa ni Mbunge wa Sengerema (CCM) aligaiwa Sh. milioni 40.4 na mfanyabiashara maarufu James Rugemalira ambaye mwanzoni mwa mwezi alifikishwa mahakamani akikabiliwa na mashtaka 12, yakiwamo ya kughushi na utakatishaji fedha.
Hata hivyo, wakati Ngeleja akithibitisha kwa risiti mbele ya waandishi wa habari kuziingiza fedha hizo katika akaunti ya TRA, mamlaka hiyo imeshasema haizitambui.
Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Tundu Lissu aliiambia Nipashe wiki iliyopita kuwa uamuzi wa Ngeleja kupeleka fedha za hizo TRA unazua maswali zaidi kwa kuwa alipewa na Rugemalira, na viongozi wa awamu ya nne ya serikali walisema siyo za umma bali mtu binafsi.
Lakini akizungumza jijini Jumatatu iliyopita Ngeleja alisema amerejesha mgawo huo kwa TRA kwa kuwa pamoja na sababu nyingine, ili kujiweka kando na kashfa.
Alisema aliyetoa mgawo huo ameshakamatwa na Takukuru na ana kesi inayoendelea katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Huku akionyesha stakabadhi ya malipo ya Benki ya CRDB tawi la Tower, Ngeleja alisema pia "nimeamua kurejesha fedha hizi hata kama aliyenipa msaada bado ni mtuhumiwa, kwa vile hajathibitika kupatikana na hatia, kwa sababu sitaki kuwa sehemu ya kashfa au tuhuma hizo."
"Nimesononeshwa na kufadhaika sana kuona kuwa msaada niliopewa sasa unahusishwa na tuhuma."
Alisema alipokea mgawo huo Februari 12, 2014 na Januari 15, 2015 alilipa kodi kwa TRA kiasi cha Sh. 13,138,125 ikiwa ni sawa na asilimia 30 ya msaada huo aliopewa.
Hakusema ni kwa nini ulipita muda mrefu kati ya kupokea na malipo ya kodi.
Post A Comment: