HUKU mashabiki wa Yanga wakiwa bado hawaamini kama kiungo Mnyarwanda Haruna Niyonzima 'Fabregas', ameshaondoka katika klabu hiyo kama inavyodaiwa, wapinzani wao Simba wanajipanga kuingiza mamilioni ya shilingi wakati wa kumtambulisha nahodha huyo wa Amavubi, imeelezwa.
Mbali na Niyonzima, Simba ambayo sasa iko chini ya Kaimu Rais, Salim Abdallah, nyota mwingine ambaye utambulisho wake unatarajia kutengeneza fedha siku hiyo kama ambavyo klabu za Ulaya zinavyofanya kwa nyota wake wapya ni Mganda Emmanuel Okwi.
Matarajio ya Simba si kutengeneza tu mamilioni ya shilingi siku hiyo ya utambulisho wa nyota hao, bali inaamini kila watakaposhuka uwanjani kwenye mechi za Ligi Kuu na kimataifa, mashabiki wataingia uwanjani kwa wingi kuwashuhudia huku wakiendelea kuuza jezi zao.
Hata hivyo, bado Simba haijatangaza rasmi kuwa imefanikiwa kumnasa mchezaji huyo wa zamani wa APR ya Rwanda mpaka pale mkataba wake na Yanga utakapomalizika mwishoni mwa wiki hii.
Taarifa kutoka Simba zinaeleza kuwa klabu hiyo inaandaa mchakato wa kisasa wa kutambulisha wachezaji wake wapya iliyowasajili ambao utaendana na thamani ya wachezaji hao husika ili kuwaenzi.
"Simba haiwezi kukurupuka, waacheni Yanga wajiulize wenyewe, wajijibu wenyewe halafu wazungumze wenyewe, nasema hii ni Simba, msimu ujao mtaipenda zaidi," alisema mmoja wa viongozi wa juu wa klabu hiyo yenye makazi yake Mtaa wa Msimbazi, Kariakoo jijini Dar es Salaam, ambaye hakuwa tayari kutajwa jina lake gazetini kwa kuwa ni kinyume cha utaratibu waliojiwekea.
Aliongeza kuwa kuanzia Jumatatu kikosi cha timu hiyo kitakuwa kimekamilika huko Afrika Kusini baada ya walioko kwenye timu ya Taifa kukamilisha jukumu la kuitumikia nchi.
"Tumesajili wachezaji kwa malengo, tunaamini kiu na ndoto zetu zitatimia na hii ni kwa ajili ya kufanya vizuri kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara na mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika tutakayoshiriki mwakani, hatutaki kuishi kwa presha, mechi zetu zote ni fainali, tumezingatia makosa tuliyofanya misimu mitatu iliyopita," aliongeza kiongozi huyo.
Tayari kikosi cha Simba kimeshaelekea jijini Johannesburg, Afrika Kusini kuweka kambi ya siku 20 kwa ajili ya kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu Bara utakaoanza kutimua vumbi ifikapo Agosti 26, mwaka huu kwenye viwanja saba hapa nchini.
Kabla ya kuanza safari ya kusaka ubingwa wa msimu 2017/18 kwa kuikaribisha Ruvu Shooting ya Pwani, Simba itavaana na mahasimu wao Yanga katika mechi ya Ngao ya Jamii itakayofanyika Agosti 23 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Post A Comment: