ads

CHAMA cha Alliance for Democratic Change (ADC), kimepongeza Serikali kwa jitihada zake za sasa za kuwachukulia hatua watu wanaotuhumiwa kwa vitendo vya ufisadi.


Pongezi hizo ilitolewa jijini Dar es Salaam juzi na Mwenyekiti wa Chama hicho, Hamad Rashid Mohamed, wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Hamad Rashid ambaye pia ni Waziri wa Kilimo, Mifugo, Uvuvi na Rasilimali katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), alisema juhudi zinazofanywa na serikali ya Rais John Magufuli zinapaswa kuungwa mkono kwa sababu zina lengo la kuwasaidia wananchi wote.

Alisema tatizo la rushwa lilikuwa limefikia katika hali mbaya, lakini serikali ya awamu ya tano imeonyesha njia ya kwamba linaweza kwisha.

“Kipindi cha nyuma rushwa ilifika mahali pabaya, watu walikuwa wanaona ni jambo la kawaida, kwa hiyo watu walikuwa wanatoa tu,” alisema na kuongeza:

“Na wengine wanapokea bila hofu na hata ulipokuwa ukilizungumzia watu hawakuelewi na wanakuona wa ajabu, lakini sasa hivi hatua zinazochukuliwa ni nzuri na haijalishi cheo au umaarufu wa mtu.”

“Kwa kweli ni jambo la kumshukuru Mwenyezi Mungu, mpaka hatua hii iliyofikia, maana kwa sasa unaweza kusimama ukazungumzia rushwa na watu wakakuelewa na pia kumekuwa na hofu sana ya kutenda mambo haya.”

Alisema hata katika SMZ, kwa sasa mapato yanayokusanywa ni makubwa tofauti na kipindi kingine chochote.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa chama hicho, Doyo Hassan Doyo, alisema msimamo wa chama hicho ni kuunga mkono endapo kunafanyika juhudi zozote zinazofanywa na serikali kwa sababu lengo lake ni kuwanufaisha Watanzania wote bila kujali itikadi zao  za vyama.

“Sisi ADC tunamuunga mkono Rais Magufuli na serikali yake katika juhudi hizi za kuwaokoa Watanzania wasiibiwe mali zao hasa kuwasilisha miswaada kwa hati ya dharura katika Bunge na kurekebisha sheria ya madini ya mwaka 2017, tunatambua kwamba juhudi hizi zitawanufaisha Watanzania wote, hivyo tumuunge mkono,” alisema Doyo.

“Kuhusu pesa zinazorejeshwa na baadhi ya waliotuhumiwa katika sakata la Akaunti ya Tegeta Escrow, sisi kwetu ni jambo jema, maana zitasaidia katika matumizi mengine ya serikali ikiwamo kuboresha huduma za jamii,” alisema.

Alisema ni vema na watu wengine waliotuhumiwa na wao wakajitafakari na kuzirejesha.
ads
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya SWAHILI NEWS kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Share To:

SWAHIBA MEDIA STAFF

Habari , karibu katika mtandao wetu ili kuhabarika na stori zote za siku katika lugha yetu adhwim ya kiswahili, habarika wakati wote weka dunia kiganjani mwako na swahili news

Post A Comment: