Ndivyo unavyoweza kusema baada ya maombi ya Kampuni ya Kufua Umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) kukwama, huku wakilazimika kuzima rasmi mitambo yao ya uzalishaji umeme.
Hatua hiyo imekuja baada ya kukwama kwa maombi ya kuongezewa muda wa miezi 55 ya leseni yake ya uzalishaji umeme kutokana na kusubiri uamuzi wa Ikulu.
Hali hiyo inajitokeza wakati mmiliki wa Kampuni ya Pan Africa Power (PAP) Harbinder Singh Sethi na Mkurugenzi wa Kampuni ya VIP Engineering, James Rugemalira wakiwa tayari wamefikishwa mahakamani kujibu mashitaka ya uhujumu uchumi, kutakatisha fedha na kusababisha hasara Serikali.
Hali za uhakika zilizolifikia gazeti hili jana zilisema mitambo hiyo kwa sasa haizalishi umeme.
MTANZANIA lilitembelea mitambo hiyo iliyoko Tegeta na kukuta wafanyakazi wachache ambao walikiri mitambo hiyo kutofanya kazi.
"Mitambo ilizimwa tangu siku ile walipomkamata Sethi", alisema mmoja wa wafanyakazi wa kampuni hiyo ambaye hakuwa tayari kutajwa jina lake gazetini.
Pamoja na hatua hiyo inaelezwa kuwa kuna hatari ya kuitaifishwa kwa mitambo hiyo hasa baada ya Serikali kuweka ngumu katika utoaji wa leseni mpya ya biashara ya kuzalisha umeme kwa kampuni hiyo.
Licha ya hali hiyo leseni ya kampuni hiyo ilimalizika muda wake Julai 15, mwaka huu ambapo hadi sasa uamuzi wa kuitaifisha mitambo hiyo kurudi kuwa mali ya TANESCO ama laa ukisubiri uamuzi wa Ikulu.
Kwa sababu hiyo, kama Serikali itaendelea na msimamo wake dhidi ya IPTL ndiyo utakuwa mwisho wa miaka 23 ya IPTL.
Kampuni hiyo au IPTL iliingia nchini tangu mwaka 1994 na kila mwezi imekuwa ikilipwa Sh. bilioni 5.943 na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) ikiwa ni gharama za uwekezaji mbali na gharama za umeme inaoliuzia shirika hilo.
Novemba 2014, baada ya Bunge kujadili Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuhusu Akaunti ya Tegeta Escrow, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), ilitoa maazimio manane ikiwa ni pamoja na kuangalia uwezekano wa kuichukua mitambo ya IPTL na kuimilikisha kwa TANESCO.
Siku chache baada ya Bunge kupitisha uamuzi huo ambao ulifanyiwa kazi kwa haraka kwa Profesa Sospeter Muhongo kujiuzulu nafasi yake.
Post A Comment: