ads

MWANASHERIA Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu amesema amepata taarifa za uhakika kuwa Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa, atafikishwa mahakamani wakati wowote kuanzia sasa na atafunguliwa mashtaka ya uchochezi.


Lissu alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mambo mbalimbali yanayoendelea ndani ya chama hicho, ikiwamo viongozi wa Chadema kukamatwa kamatwa na Jeshi la Polisi.

Lissu alisema amepata taarifa hizo jana kutoka katika chanzo cha kuaminika ndani ya Jeshi la Polisi kwamba tayari utaratibu wa kumfikisha Lowassa mahakamani uko katika hatua za mwisho.

Mara tatu Lowassa ambaye alikuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chadema akiungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ameitwa Makao Makuu ya Polisi jijini Dar es Salaam kwa mahojiano juu ya kauli inayodaiwa kuwa ya uchochezi.

Lowassa ambaye aliwania urais kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na kuungwa mkono na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, anadaiwa kutoa maneno ya uchochezi jijini wakati wa hafla ya futari iliyoandaliwa na Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara (Chadema).

Katika hafla hiyo, Lowassa alimtaka Rais John Magufuli kutafakari upya hatima ya masheikh wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (Jumuki), maarufu Uamsho, wanaoshikiliwa mahabusu kwa zaidi ya miaka minne wakikabiliwa na mashtaka ya ugaidi.

Alisema ni jambo la fedheha kwa nchi iliyopata uhuru zaidi ya miaka 50 kuwaweka mahabusu viongozi wa dini bila kesi kusikilizwa mahakamani.

Kutokana na matamshi hayo, DCI alimwandikia barua ya kumhitaji kwa mahojiano.

“Nimepata taarifa tena kwa polisi mwenye cheo kikubwa tu ndani ya Jeshi hilo kwamba utaratibu unafanywa wa kumfikisha Lowassa mahakamani na watamshtaki kwa kosa la uchochezi,” alisema Lissu makao makuu ya Chadema, Mtaa wa Togo, Manispaa ya Kinondoni.

“Nimeambiwa jiandaeni, Lowassa atapelekwa mahakamani, kwa hiyo hii ndiyo taarifa niliyopata,” alisema Lissu.

Lissu alipoulizwa kuhusu kinga ya kiongozi kama huyo aliyewahi kushika nafasi kubwa serikalini, alisema kwa mujibu wa sheria za nchi zilizopo, hakuna kiongozi mwenye kinga dhidi ya kosa la jinai zaidi ya Rais.

“Kwa mujibu wa Sheria za Tanzania, mtu pekee ambaye ana kinga dhidi ya mashtaka ya jinai ni Rais pekee, wengine wote kuanzia Makamu wa Rais mpaka karani wote wanashtakiwa,” alisema.

“Na kwa mantiki hiyo, hata Lowassa akipelekwa mahakamani hataweza kusema aliwahi kuwa Waziri Mkuu. Hata Rais mwenyewe kinga yake inafanya kazi pale anapoapishwa na kipindi kile chote atakachokuwa madarakani, lakini anapomaliza, makosa yote ya jinai atakayofanya kipindi anachokuwa nje ya madaraka hana kinga.”

Rais John Magufuli alionya wanasiasa wanaowatetea masheikh wa Uamsho, wanaokabiliwa na kesi ya uhaini mahakamani wakati wa halfa ya uwekaji wa jiwe la msingi la mradi wa uboreshaji wa Bandari ya Dar es Salaam utakaoghalimu dola za Marekani milioni 421 (sawa na Sh. bilioni 926.2), Julai 2.

Rais Magufuli alivitaka vyombo ya dola kuwakamata wale wote wanaotoa kauli za kutetea Uamsho ili wakaisaidie polisi katika uchunguzi bila ya kuangalia "anatembea taratibu, haraka, wala cheo alichonacho".

ZITOE AMRI
Wakati huo huo, Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu awaambia waandishi wa habari kuwa Katibu Mkuu wa Chama hicho, Dk. Vicent Mashinji, pamoja na viongozi wengine wa chama hicho waliokuwa wakishikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Ruvuma wameachiliwa kwa dhamana.

“Hatimaye Katibu Mkuu Dk. Mashinji na viongozi wengine nane wakiwamo wabunge wawili wameachiwa huru," alisema Lissu.

"Jana (juzi) tulizitaka mamlaka zilizohusika kutoa amri ya kuwakamata zitoe amri ya kuwaachia huru kabla chama hakijatoa kauli kuhusu hatua nyingine ambazo kingezichukua, kwa hiyo leo wametolewa, ila wamesema kesho wanatakiwa tena kwenda kuripoti, lakini haijulikani wanakwenda kuripoti kwa nani,” alisema Lissu.

Viongozi wengine waliokuwa kizuizini tangu Jumamosi mkoani Ruvuma ni Mwenyekiti wa Kanda ya Kusini na Mbunge wa Jimbo la Ndanda, Cecil Mwambe, Katibu wa Kanda, Philbert Ngatunga, Ofisa wa Operesheni na Mafunzo, Manawa Samuda na Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Ruvuma, Zubeda Sakuru.

Wengine ni Ofisa wa Kanda ya Kusini, Asia Mohamed, Mwenyekiti wa Mkoa wa Ruvuma, Ireneus Ngwatura, Katibu wa Mkoa wa Ruvuma Delphin Ngaiza, Mwenyekiti wa Wilaya ya Nyasa, Cuthbert Ngwata na Katibu Mwenezi wa Wilaya ya Nyasa, Charles Makunguru.

Ilidaiwa kuwa viongozi hao walikamatwa baada ya kuvamiwa gafla na askari katika kikao cha ndani kilichokuwa kikiendelea mjini Nyasa mkoani Ruvuma ikiwa ni sehemu ya ziara ya Katibu Mkuu huyo kukagua shughuli za chama katika majimbo ya Kanda hiyo.

Wakati huo huo, Daniel Limbe, Chato anaripoti kuwa viongozi na wafuasi 51 wa (Chadema) wameendelea kusota rumande katika Gereza la Biharamulo mkoani Kagera baada ya jana kushindwa kupewa dhamana.

Wanakabiliwa na kesi ya kufanya mkusanyiko bila ya kuwa na kibali kwenye kata ya Muganza wilayani Chato mkoani Geita na wapo ndani tangu Julai 7 walipokamatwa kwenye ukumbi wa Manzagata.

Jana, hata hivyo, palizuka mvutano mkali wa kisheria kati ya upande wa mashtaka na wakili wa utetezi ambaye aliomba kuondolewa zuio la wateja wake kupewa dhamana kabla kesi ya msingi haijasikilizwa.

Kutokana na hali hiyo, Hakimu wa mahakama ya Wilaya ya Chato, Jovith Kato, alizipa dakika 15 za majadiliano pande hizo ili kuona namna bora ya uwasilishaji wa hoja zao, iwapo waendelee kwa maneno au kwa maandishi.

Baada ya mazungumzo hayo, pande hizo zilikubaliana kujibizana kwa maandishi ambapo upande wa mashtaka uliomba kupewa pingamizi lililowekwa na wakili wa washtakiwa, Edward John, ili waweze kuzijibia hoja zilizoandikwa.

Upande wa mashtaka uliokuwa ukiwakilishwa na Mwendesha Mashtaka, Semen Nzigo, uliomba mahakama hiyo kupitia pingamizi hilo kabla kuwasilisha majibu ya upande wa washtakiwa.

Baada ya pande hizo mbili kuafikiana, Hakimu Kato, aliutaka upande wa mashtaka kuwasilisha majibu ya pingamizi hilo kabla ya Alhamisi ambapo hoja zote zitapitiwa na kutolewa uamuzi wa awali.

Wakati mvutano huo wa kisheria ukiendelea, washtakiwa wote hawakuwapo mahakamani kwa madai kwamba Jeshi la Polisi wilayani hapa lilikosa gari la kuwafuata kwenye Gereza la Biharamulo.

Baadhi ya viongozi hao walioko gerezani ni pamoja na Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Geita, Phabian Mahenge, Katibu wa Chadema Mkoa huo, Sudy Tuganyala, Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Mkoa, Vitus Makoye na Mwenyekiti wa Bavicha Mkoa huo, Neema Chozaile.

Wengine ni Katibu wa Chadema Wilaya ya Chato, Mange Ludomya, Kaimu Mwenyekiti Chadema Wilaya ya Chato, Uhuru Selemani, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji wa Wilaya hiyo, Meshark Tulasheshe na Katibu Mwenezi Kata ya Muganza, Marko Maduka ambaye pia alikuwa diwani wa Chadema awamu iliyopita.

BILA KUANGALIA

Ni mara ya tatu kwa Lowassa kujikuta mikononi mwa Polisi baada ya kukamatwa kwa mara ya kwanza jijini Dar es Salaam Agosti 29, mwaka jana na baadaye msafara wake kuzuiwa kwa saa kadhaa mkoani Geita Januari 16, mwaka huu.

Alipokamatwa na kuhojiwa Kanda Maalumu ya Polisi Dar es Salaam Agosti mwaka jana, Lowassa na viongozi wa juu watano wa Chadema walidaiwa kufanya mkutano wa ndani wa chama bila kibali.

Kwenye tukio la pili la Januari mwaka huu, Jeshi la Polisi mkoani Geita lilieleza kuwa liliamua kuuzuia kwa muda msafara wake uliokuwa unatoka Kagera kwenda Mwanza kutokana na kitendo chake cha kusimama njiani na kuzungumza na wananchi bila kibali.

Credit - Nipashe
ads
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya SWAHILI NEWS kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Share To:

SWAHIBA MEDIA STAFF

Habari , karibu katika mtandao wetu ili kuhabarika na stori zote za siku katika lugha yetu adhwim ya kiswahili, habarika wakati wote weka dunia kiganjani mwako na swahili news

Post A Comment: