Mbunge wa Viti maalum (CUF) Mgeni Kadika ambaye ni miongoni mwa wabunge wawili wa chama hicho ambao wanadaiwa kusamehewa na Baraza Kuu la Chama cha Wananchi CUF (Upande wa Prof. Lipumba) kutokana na kuitika wito.
Mgeni Kadika amekanusha vikali taarifa za viongozi hao na kusema yeye hakuitika wito wala kutoa udhuru kwa viongozi walio chini ya Profesa Lipumba na ameahidi kuongozana na wabunge wengine 8 katika kila hatua watakayokwenda kwani yeye hautambui uongozi wa Lipumba.
"Mimi sielewi kwanini nimebaki na sijafukuzwa kama ambavyo wameyatangaza, ingawa nasikia wanasema kuwa nilitoa dharura mimi nakanusha sikutoa dharura yoyote ile kwao sababu mimi ni mzima wa afya njema na watoto wangu wazima, nasema hivi mimi siendi hata siku moja kwao ila wenzangu hawa 8 ambao wanadaiwa kufukuzwa watakapokwenda tutakuwa pamoja na tukiondoka tutaondoka pamoja, mimi siwezi kusaliti chama changu cha CUF" alisisitiza Mgeni
Hata hivyo Mbunge wa Viti Maalum na Kiongozi wa Wabunge wa CUF bungeni, Riziki Ngwali ambaye ni miongoni mwa wabunge 8 waliofukuzwa uanachama na Baraza Kuu la Chama cha Wananchi (CUF) lilochini ya Lipumba amefunguka na kusema wao watakwenda mahakamani kudai haki yao.
"Huu uamuzi tumeusikia tu ila rasmi bado hatujapata barua kwa sababu sisi tuliteuliwa kwa barua na matarajio kwamba tutatenguliwa kwa barua lakini vyovyote itakavyokuwa hatukubaliani na uamuzi huu ambao si halali kwa sababu umetoka katika mamlaka ambayo si halali, saizi kinachofuata ni kwenda mahakamani kwa sababu ni haki ambayo sisi tumedhulumiwa na kunyang'anywa kwa hiyo sisi tutakwenda mahakamani kutafuta haki" alisema Riziki Ngwali
Aidha Mwenyekiti wa kamati ya muda ya uongozi CUF, Julius Mtatiro amewataka wanachama wa chama hicho cha CUF kuendelea kuwa watulivu na kudai kuwa Profesa Lipumba sasa amechanganyikiwa na kusema licha ya mambo yote anayoyafanya lakini hawezi kufanikiwa kukiyumbisha chama hicho.
Post A Comment: