RAIS John Magufuli ameagiza kikosi kazi cha kupambana na ujangili,
kutafuta na kukamata watu wote wanaoua tembo, ikiwemo walioua tembo
ambao pembe zao zimekamatwa Dar es Salaam.
Alisema hayo alipofanya ziara ya kushtukiza katika Ofisi za Wizara ya
Maliasili na Utalii (Mpingo House), jijini Dar es Salaam kwa lengo la
kufuatilia utekelezaji wa operesheni ya kukabiliana na ujangili,
inayofanywa na Kikosi Kazi kilichoundwa na wizara hiyo.
Taarifa iliyotolewa na Ikulu, Dar es Salaam jana, ilisema akiwa
katika ofisi hizo jana Rais Magufuli aliyekuwa na Katibu Mkuu wa Wizara
ya Maliasili na Utalii, Meja Jenerali mstaafu Gaudensi Milanzi
alishuhudia pembe 50 za ndovu zilizokamatwa kati ya juzi na jana jijini
Dar es Salaam.
Aidha, Rais Magufuli alioneshwa magari yaliyokamatwa yakiwa yamebeba
pembe hizo na watuhumiwa wanane, wanaodaiwa kujihusisha na mtandao wa
biashara haramu ya pembe za ndovu.
Rais aliwapongeza askari wote waliopo katika Kikosi Kazi cha
kudhibiti na kupambana na biashara haramu ya pembe za ndovu pamoja na
raia wema wote, wanaotoa ushirikiano katika operesheni hiyo na
aliwahakikishia kuwa anatambua kazi kubwa wanayoifanya na anawaunga
mkono.
“Nawapongeza sana kwa kazi nzuri mnayoifanya na ninawahakikishia kuwa
ninawaunga mkono, chapeni kazi, wakamateni wote wanaojihusisha na
biashara hii haramu, hakuna wa kumbakiza, awe mkubwa au nani, kamateni,
wala msijali cheo chake, umri wake, dini yake, kabila lake, umaarufu
wake, sheria ni msumeno.
“Watafuteni wote mpaka watu wakiona tembo wawe wanakimbia wenyewe ili
tuokoe wanyama wetu ambao wanaendelea kuteketezwa. “Hapa mmekamata
pembe 50 maana yake tembo 25 wameuawa, haiwezekani maliasili yetu ikawa
inapotea hovyo hovyo kwa sababu ya watu wachache wenye tamaa ya kutaka
utajiri wa haraka haraka,” alisisitiza Rais Magufuli.
DOWNLOAD
APP YETU YA SWAHIBA NEWS ILI UWEZE KUPATA HABARI ZOTE MOJA KWA MOJA
KUPITIA SIMU YAKO YA MKONONI BILA KUINGIA KWENYE WEBSITE,KUDOWNLOAD
BONYEZA HAPA
ANDIKA MAONI YAKO HAPO CHINI
Post A Comment: