ads

SASA hii ni jeuri ya fedha, kwani baada ya Simba kufanikiwa kuzinasa saini za John Bocco, Shomari Kapombe na kipa Aishi Manula kutoka Azam FC, mwanachama maarufu wa Wekundu hao wa Msimbazi, Mohammed Dewji ‘Mo’, ameuambia uongozi utafute wachezaji wengine wazuri, kwani fedha kwake si tatizo.


Mbali na wachezaji hao watatu kutoa Azam FC, pia Simba imefanikiwa kuzinasa saini za mabeki wawili, Jamal Mwambeleko kutoka Mbao FC pamoja na Yussuf Mlipili kutoka Toto Africans, zote za jijini Mwanza, na Mo amesema anataka waletwe wengine wenye uwezo mkubwa zaidi.

Gazeti la Dimba limenasa ujumbe wa Mo ukiwataka Wanasimba kuwa kitu kimoja, huku akisisitiza kwamba lazima ufanyike usajili wa nguvu ili timu irudishe heshima yake iliyopotea kwa misimu kadhaa.

“Narudisha heshima ya Simba SC iliyopotea ndani ya misimu mitatu, pesa si tatizo kwangu, usajili huu ni chachu ya Simba kuelekea kwenye mafanikio endelevu na kufanya vyema kimataifa, huu ni muda mzuri kwetu kuunganisha nguvu zetu zote kuona Simba SC inafanikiwa na kuliletea heshima taifa letu, Simba nguvu moja,” ulisomeka ujumbe huo.

Kauli hiyo ya Mo inaupa uongozi jeuri ya kuinasa saini ya mastraika hatari kutoka nje ya nchi, akiwamo yule straika wa Zambia, Walter Bwalya, ambaye ana njaa ya mabao kinoma.

Aidha, Mo, ambaye ameonekana kujiamini sana, amewahakikishia Wanasimba kwamba mbali na huyo, pia straika mwenye zali na Simba, Emmanuel Okwi, wanamalizana naye kila kitu ndani ya siku mbili hizi na atatua Msimbazi dakika yoyote kuanzia sasa, huku pia klabu hiyo ikikamilisha mazungumzo na straika wa AFC Leopards, Allan Kateregga, ambaye wamekuwa wakimfukuzia baada ya kuona uwezo wake katika michuano ya SportPesa, iliyomalizika hivi karibuni Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam.

Mbali na Kateregga, pia huo utakuwa mwanya kwa uongozi kumpelekea mapendekezo yao juu ya uhitaji wa wachezaji wawili kutoka Yanga, Donald Ngoma pamoja na Haruna Niyonzima, ambao wamekuwa wakiwafukuzia, hasa baada ya mikataba yao na Yanga kufikia ukingoni.

Uongozi wa Wekundu hao wa Msimbazi umekuwa kwenye mipango kabambe ya kutaka saini za Ngoma na Niyonzima, ila tatizo linakuja kwenye fedha wachezaji hao wanazozitaka za usajili, lakini sasa viongozi hao wanaweza wakampelekea Mo mezani kwake, ambapo atazungumza na mastaa hao na kumalizana nao kiutu uzima.

Anachokifanya Mo kinaendana na kile kikao kizito kilichokaliwa mjini Dodoma kati ya uongozi na baadhi ya wabunge na mawaziri wanaoshabikia Simba, baada ya kumalizika kwa mchezo wa fainali ya michuano ya Kombe la FA, ambapo Wekundu hao wa Msimbazi walifanikiwa kuwafunga Mbao bao 1-0, ambapo kikao hicho kwa kauli moja kiliafikiana kuifumua timu na kuijenga upya, hasa kwa kununua wachezaji wenye uwezo mkubwa.

Vigogo hao walipendekeza usajili wao uzingatie uwezo wa mchezaji husika na kubwa zaidi mwenye uzoefu wa michuano ya Kimataifa, hiyo ikiashiria kuwa ni maandalizi ya kukijenga kikosi chao katika mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika, ambayo watashiriki mwakani.

Wanachotaka kukiona Vigogo hao ni ile Simba ya mwaka 2003, iliyokuwa na mafanikio makubwa ndani na nje ya nchi, hasa ikiweka historia ya kuwatupa nje ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika waliokuwa mabingwa watetezi wa michuano hiyo, Zamalek ya nchini Misri.
ads
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya SWAHILI NEWS kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Share To:

SWAHIBA MEDIA STAFF

Habari , karibu katika mtandao wetu ili kuhabarika na stori zote za siku katika lugha yetu adhwim ya kiswahili, habarika wakati wote weka dunia kiganjani mwako na swahili news

Post A Comment: