ads

MBUNGE wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM), amesema Serikali isipoifutia leseni ya uchimbaji madini Kampuni ya Mwabangu, ataungana na wananchi na kuwaruhusu wang’oe mabati katika Chuo cha Madini wagawane.


Wakati Bashe akisema hayo, Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche (Chadema), amesema atahamasisha wananchi wakachukue kilicho chao kwenye mgodi wa Acacia, huku Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM), akishangaa kwa nini hadi sasa polisi na jeshi hawajaenda kwenye mgodi huo.

Akichangia bajeti kuu ya Serikali ya mwaka 2017/18, Bashe alisema: “Naomba kuwaambia wabunge wenzangu, Watanzania wanapokwenda kuchagua viongozi na wanapokwenda kupiga kura ya kumchagua rais, wanamkabidhi dhamana juu ya uhai wao, usalama wao, anakuwa mlinzi wa rasilimali zao walizopewa na Mungu.

“Rais ameunda tume mbili na ametusomea matokeo ya tume, lakini nyuma marais waliotangulia nao waliunda tume mbalimbali, vita ya kupambania rasilimali za nchi hii si ya Rais Magufuli peke yake, ni ya Watanzania wote, hakuna kufanya kosa katika kufanya jambo jema.

“Bunge limefanya makosa, viongozi wetu wamefanya makosa, leo tumepata mtu wa kupigania rasilimali zetu, tumuunge mkono, akishindwa kutufikisha mwisho tumnyooshee mkono.

“Kule Nzega, Kigwangala alipigwa mabomu kwa ajili ya Mgodi wa Resolute, tumeibiwa. Kama alivyosema Heche, niungane naye, Kule Nzega Resolute kaondoka na Sh bilioni 10 za kodi ya huduma, wameacha mashimo… Serikali imeipa Kampuni tanzu ya Resolute, Mwabangu Mining leseni ya kuchimba madini, wallahi wabillahi nitaongoza wananchi bila kujali kitakachotokea kama leseni haitafutwa.

“Resolute wana mgogoro wa kodi na TRA, nataka katika majumuisho mniambie kuhusu Sh bilioni 10 za Nzega tutazipataje.

“Nitamuunga mkono Rais Magufuli katika jitihada zake zote, kile chuo mlichofungua cha madini naenda kuwaambia wananchi wang’oe mabati wagawane.

“Rais kawa mstaarabu sana, angetangaza kufunga migodi, Mgodi wa Diamond William, pembeni kuna uchimbaji mwingine unaendelea wa Kampuni ya Hillary, wanachukua dhahabu Mgodi wa Mwadui wanaenda kuyatengenezea katika Mgodi wa Hillary,” alisema Bashe.

Kwa upande wake, Lugola alisema Magufuli wa leo si wa jana.

“Rais Magufuli wa leo tofauti na wa jana, Magufuli wa leo tunamzungumzia kikatiba, ni Rais na Amiri Jeshi Mkuu, inakuwaje mtu anakuwa na mashaka na uamuzi wake na utendaji wake.

“Nilitegemea mawaziri waanze kazi kwa kwenda katika migodi kuzuia dhahabu, mnasubiri nini, mnahangaika na wawekezaji, mafisadi wamepatikana bado tunasota, eti tunajadiliana na wezi… tunajadiliana nini… mtakaa nao Bahari Beach Hotel katika kiyoyozi, mahakama ya mafisadi ipo hawapelekwi,” alisema Lugola.

Akichangia bungeni juzi, Mbunge wa Tarime Vijijini, Heche, alisema kwa sababu ripoti imeonyesha kuwa Kampuni ya Acacia haijasajiliwa nchini na hivyo haitambuliki, sasa ni muda wa kuhamasisha wananchi wakachukue kilicho chao katika mgodi huo.

“Kwamba Acacia ni kampuni feki, ni kampuni hewa ambayo haipo, lakini ipo Tarime na inawaibia wananchi wa Tarime, kuanzia leo nawaambia wananchi wa Tarime wajiandae tuingie mle mgodini tuchukue kila kilicho chetu.

“Na mimi hili nalisema humu, na nitalifanyia kazi na sidanganyi kwa sababu wananchi wa Tarime wameumizwa na kampuni ile.

“Sisi watu wetu (wananchi wa Tarime), mheshimiwa Spika unajua, wewe ukiwa Naibu Spika, wameumia na maji ya sumu, ng’ombe wamekufa, watu wamepigwa risasi, kwa mujibu wa ripoti ya Waziri wa Nishati na Madini.

“Watu wa Tarime zaidi ya 64 wameuawa na hao ni kwa mujibu wa ripoti ya waziri mwenyewe, wameuawa pale mgodini Serikali ikilinda hawa wezi wa Acacia, ndiyo maana tunasema watu wengine tuna machungu na tuna maumivu na hili,” alisema.
ads
Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya SWAHILI NEWS kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Share To:

SWAHIBA MEDIA STAFF

Habari , karibu katika mtandao wetu ili kuhabarika na stori zote za siku katika lugha yetu adhwim ya kiswahili, habarika wakati wote weka dunia kiganjani mwako na swahili news

Post A Comment: