Sakata la utekaji limeendelea kung’ang’ania bungeni baada ya mbunge wa Ukonga (Chadema), Mwita Waitara kutaja wabunge watano akidai kuwa wamo kwenye orodha ya watu wanaotakiwa na Idara ya Usalama wa Taifa.
Amesema hayo siku moja baada ya mbunge wa Nzega Mjini (CCM), Hussein Bashe kukiambia chombo hicho kuwa alitekwa na maofisa wa idara hiyo wakati akitoa taarifa baada ya mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe kutakiwa atoe uthibitisho kuwa Usalama wa Taifa wanahusika na utekaji watu unaoendela nchini.
Akizungumza wakati wa kuomba mwongozo bungeni jana, Waitara alisema kuna timu mbili za watu watatu zimeundwa na Usalama wa Taifa kwa ajili ya kuteka watu.
“Jana (juzi) nikiwa hapo nje nilipokea message (ujumbe) kuhusu wabunge ambao ni target (walengwa). Mtoa taarifa anasema zimeundwa timu mbili za watu watatu za Usalama wa Taifa,” alisema.
Alitaja wabunge ambao wanatafutwa kuwa ni Nape Nnauye (Mtama-CCM), Hussein Bashe (Nzega Mjini-CCM), Godbless Lema (Arusha Mjini-Chadema), Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini-Chadema) na yeye mwenyewe.
Post A Comment: