MKUU wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Ernest Mangu, kwa mara ya kwanza amezungumza kuhusu vinavyodaiwa kuwa vitendo vya utekwaji na upoteaji wa watu maarufu hapa nchini, akisema mwenye ushahidi juu ya kutekwa kwa Ben Saanane ajitokeze.
Katika mazungumzo yake na Raia Mwema yaliyofanyika juzi Jumatatu, IGP Mangu alisema Tanzania haina tatizo la watu kutekwa au kutoroshwa isipokuwa kuna watu wanalikuza kwa sababu zao binafsi.
Kauli hii ya askari polisi namba moja nchini, imekuja katika kipindi ambacho taifa liko katika fukuto la kupotea na kutekwa kwa watu wawili maarufu nchini; mmoja mwanasiasa na mwingine msanii.
Juzi Jumatatu, Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe, aliomba Bunge liahirishe mijadala mingine inayoendelea ili kwamba jambo hili la watu kutekwa au kupotea katika mazingira tatanishi lizungumzwe kwa kina.
Lakini, Mangu alisema kwa kadri rekodi za polisi zinavyoonyesha, Tanzania haina rekodi mbaya ya matukio hayo kama ambavyo inasemwa na baadhi ya watu.
“Mimi ni askari na naweza kukwambia kwamba tuna kesi nyingi tu za watu waliopotea. Kama wewe ni mwangaliaji mzuri wa vipindi vya televisheni saa za jioni, utakuwa unaona matangazo ya watu waliopotea.
“ Mtu kupotea kuna sababu nyingi. Si lazima apotee kwa kutekwa. Kuna wengine wana matatizo yao ya kisaikolojia na yanawasababishia kupotea. Tatizo ni kwamba ninyi (vyombo vya habari) mnabagua. Watu wengine wakipotea hamsemi, wengine wakipotea mnasema.
“ Sisi hatubagui. Haki ya kuishi ya raia wote wa Tanzania ni sawa kwa mujibu wa Jeshi la Polisi. Wote waliopotea tunawatafuta na kuwapa uzito sawa. Sisi hatuna ubaguzi wa raia maarufu na wasio maarufu au wasanii na wasanii na wasio wasanii.
“Kwenye suala la kutekwa, hebu niambie, nani ambaye unamfahamu alitekwa? Alitekwa na nani? Ushahidi kwamba alitekwa uko kwa nani,” alihoji Mangu.
Kuhusu Ben Saanane
Mangu, kwa mara ya kwanza, alizungumza pia kuhusu kupotea kwa aliyekuwa Mkurugenzi wa Utafiti na Sera wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Benard (Ben) Rabiu Saanane ambaye pia alikuwa mwanasafu wa gazeti hili la Raia Mwema.
Katika mazungumzo yake na gazeti hili, Mangu alisema Jeshi la Polisi bado linaendelea na msako wake wa kumtafuta Saanane na kwamba hadi sasa hakuna sababu ya kutuhumu upande wowote kutokana na kutoweka huko kwa mwanasiasa huyo.
Saanane hajaonekana hadharani tangu Novemba 18 mwaka jana lakini Mangu alisema wameomba kila aina ya ushirikiano kutoka sehemu mbalimbali katika kuhakikisha kuwa kijana huyo anapatikana.
“ Jambo moja la uhakika ambalo naweza kukwambia ni kwamba sisi tunamtafuta Ben Saanane kwa nguvu zote. Hadi sasa hakuna ushahidi kwamba alitekwa na hivyo sisi tunamtafuta kama missing person (mtu aliyepotea). Kama kuna mtu ana ushahidi kuwa bwana Saanane alitekwa basi aje nao kwetu na sisi tutaufanyia kazi,” alisisitiza Mangu.
Kuhusu Roma Mkatoliki
Msanii mashuhuri wa muziki wa kizazi kipya, Ibrahim Mussa, maarufu kwa jina la Roma Mkatoliki, alidaiwa kutekwa jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki iliyopita, ingawa alipatikana na kuzungumza na wanahabari juzi Jumatatu.
Hata hivyo, Mangu alisema kwa sababu Roma mwenyewe anapatikana, ni vema akaulizwa kama alitekwa au la na kama ni kweli, alitekwa na kina nani.
“ Sitaki kuzungumzia suala la huyo kijana kwa sababu yeye mwenyewe yupo. La Saanane nimelizungumza. Huyo Roma yupo na umuulize na majibu yake yatakueleza kama alitekwa au la,” alisema Mangu.
Katika mazungumzo yake na waandishi wa habari katika ukumbi wa Idara ya Habari (Maelezo) jijini Dar es Salaam juzi, Roma hakuweka bayana nini kilichotokea zaidi ya kusema alitekwa na watu wasiojulikana.
Msanii huyo aliyezua mijadala katika vyombo vya habari na mitandao ya kijamii nchini, hakutaka kuingia undani wa sakata lake hilo zaidi ya kusema kwamba suala hilo linachunguzwa na Polisi na yeye hataki kuingilia uchunguzi huo.
Kuna watu wanakuza tu haya mambo kwa sababu wanazozijua wao wenyewe. Tanzania hakuna tatizo la watu kutekwa wala kupotezwa na makundi ya wahalifu au vyombo vya dola. Hilo tatizo halipo.
“Kwa mambo ambayo tayari yamefika Polisi, ingekuwa vyema kwa jamii kuacha wenye utaalamu wa kuchunguza wafanye kazi yao.
Msimamo wa Chadema
Saanane alikuwa mmoja wa wasaidizi wa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, na ingawa chama hicho hakikutoa taarifa mapema kuhusu kupotea kwa Ben, hatimaye mbunge huyo wa Hai alitoa maelezo yake kuhusu jambo hilo.
“Ndugu zangu Watanzania, msione nipo kimya, nimefanya hivi kutokana na kuwa suala hili lipo kwenye uchunguzi kwani tukizidisha kuongea ongea wale ambao wamemteka wanaweza kupoteza uhai wake kisa maneno. Chadema ni taasisi ambayo ina vyombo vyake vya ulinzi na usalama ambavyo vinaendelea kuchunguza tukio hili la aina yake, alisema.
Mbowe alisema hayo wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Mbeya Desemba 24 mwaka jana, wakati wa uchaguzi wa viongozi wa chama hicho Kanda ya Nyasa inayojumuisha mikoa ya Iringa, Mbeya, Songwe, Njombe na Rukwa.
Alisema yeye pia ameathiriwa na tukio hilo kama ilivyo kwa wazazi wake na ndugu wengine kwa kuwa ni mtu muhimu kwake katika kutekeleza majukumu yake.
Kabla ya Mbowe kuzungumza na wana habari, kundi la Umoja wa Kizazi cha Kuhoji Tanzania (UTG) lilizungumza na waandishi wa habari kueleza rasmi kuhusu kupotea kwa Saanane na hatua walizokuwa wamechukua kufuatilia hatma yake.
“Mnamo Novemba 18 mwaka huu (2016), Katibu wa kundi hili, Benard Saanane au maarufu kama Ben Saanane aliondoka nyumbani kwake maeneo ya Tabata jijini Dar es Salaam, na tangu siku hiyo hajaonekana tena hadi leo yapata siku 24.
“Tukio la kupotea kwa Ndugu Saanane lilianza kuibua mijadala kuanzia Novemba 26 mwaka huu baada ya Ben kutokuonekana nyumbani kwake Tabata, na katika eneo lake la kazi ambalo ni Makao makuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeo (Chadema).
“Baada ya siku kadhaa za kutokujulikana alipo, familia yake ikawasiliana na watu mbalimbali wa karibu na Ben kujua kama wana taarifa yoyote kuhusu Ben alipo.
“Tunakitaka Chadema ambayo ndiyo taasisi Saanane aliyokua akiifanyia kazi, kuchukua hatua za kiridhisha dhidi ya suala hili. Sisi kama UTG hatujaridhishwa na namna chama hicho kinavyochelewa kuchukua hatua. Ben amekua mtumishi wa Chadema wa muda mrefu, hivyo hatuoni kama ni sahihi kwa chama hicho kushindwa kutoa tamko lolote hadi leo, ikiwa ni siku 24 sasa tangu apotee.
“Tunazitaka taasisi zote za haki za binadamu zijitokeze hadharani na kupiga kelele juu ya mambo haya mawili makubwa katika taifa. Zipige kelele Ben apatikane akiwa hai,” lilieleza kundi hilo kupitia kwa Mwenyekiti wake, Godlisten Malisa.
Credit - Raia Mwema
Post A Comment: