Kama kuna watu walifikiri Rais John Magufuli hajui fasihi, basi wamejidanganya kwani jana alionekana kujibu kiaina wimbo wa kundi la wanamuziki wa rap la Wagosi wa Kaya unaoitwa ‘Dereva’.
Rais Magufuli alijifananisha na dereva wa lori ambaye “hawezi kusikiliza nyimbo za abiria” unaoitwa “Dereva”.
Alitoa kauli hiyo wakati akizindua awamu ya kwanza ya ujenzi wa reli ya kisasa kati ya Dar es Salaam na Morogoro, itakayotumiwa na treni ya umeme katika hafla iliyofanyika Pugu jijini Dar es Salaam.
Wakati Wagosi wa Kaya wanamfananisha kiongozi wa sasa na dereva wa basi asiyesikiliza abiria wake, Rais Magufuli alijifananisha na dereva wa lori aliyechukua abiria wa aina tofauti.
Katika wimbo huo, Wagosi wa Kaya wameelezea viongozi wa Serikali katika awamu zote nne ambao wamekuwa wakisikiliza abiria wao wanapokuwa na shida, lakini wanasema wa awamu ya tano hasikilizi abiria hata wanapotaka kushuka kujisaidia.
“Unapopakia abiria kwenye lori, huhitaji kuwauliza watasimama sehemu gani wakati lori linaondoka. Wapo watakaotazama nyuma, wapo watakaotazama ubavuni, wapo watakaotazama ubavu mwingine, wapo watakaotazama kule lori unakolipeleka ili lifike salama. Lakini wapo wengine, kama utakuwa umepania wasukuma, watakuwa wanaimba,” alisema Magufuli.
Post A Comment: