WAFUASI 22 wa Kundi la ‘Blue Guard’ la Chama cha Wananchi (CUF)
wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini
Dar es Salaam wakikabiliwa na mashitaka manne likiwemo la kukutwa na
silaha za Jeshi la Polisi.
Washitakiwa hao ambao ni wakazi wa Zanzibar walifikishwa mahakamani
hapo jana na kusomewa mashitaka na Wakili wa Serikali, Patrick Mwita
mbele ya Hakimu Mkazi, Godfrey Mwambapa.
Mwita alidai, washitakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka manne ya kula
njama, kuingilia majukumu ya kipolisi kupitia genge la uhalifu pamoja
na kukutwa na silaha pamoja na zana za Jeshi la Polisi.
Akisoma mashitaka, Wakili Mwita alidai, kati ya Septemba 20 na 25,
mwaka huu kati ya Zanzibar na Dar es Salaam, kupitia kikundi cha Blue
Guard, washitakiwa na wenzao ambao hawakufikishwa mahakamani walikula
njama za kuajiri watu, wafanye kazi za kipolisi kinyume cha Sheria ya
Makosa ya Jinai.
Aliendelea kudai kuwa, washitakiwa wakiwa wanachama wa kundi la Blue
Guard waliwaajiri watu kwa ajili ya kufanya kazi za Kipolisi kinyume na
sheria.
Wakili Mwita alidai, Septemba 25, mwaka huu katika eneo la
Mwananyamala, Dar es Salaam, wakiwa na lengo la kutenda kosa,
washitakiwa walikutwa wakiwa na silaha kinyume cha sheria , ikiwemo visu
vitano pamoja na mabomu ya machozi 10 kwa ajili ya kuyatumia katika
uvamizi.
Aidha, inadaiwa siku hiyo hiyo, Dar es Salaam, washtakiwa walikutwa
wakiwa na zana za Jeshi la Polisi ambazo ni mabomu ya machozi
yanayotumiwa na jeshi hilo katika majukumu yao.
Baada ya kusomewa mashitaka washitakiwa hao walikana kutenda makosa
hayo, hata hivyo Wakili Mwita alidai upelelezi wa kesi hiyo bado
haujakamilika na kuomba wapangiwe tarehe nyingine ya kutajwa.
DOWNLOAD
APP YETU YA SWAHIBA NEWS ILI UWEZE KUPATA HABARI ZOTE MOJA KWA MOJA
KUPITIA SIMU YAKO YA MKONONI BILA KUINGIA KWENYE WEBSITE,KUDOWNLOAD
BONYEZA HAPA
ANDIKA MAONI YAKO HAPO CHINI
Post A Comment: