WAKATI kelele za matarajio makubwa kutoka
kwa mashabiki kupitia vyombo vya habari zikielezwa kuwa chanzo cha
kiungo wa Manchester United, Paul Pogba, kushindwa kuonyesha kiwango
chake, mshambuliaji wa Yanga, Amissi Tambwe, amempa siri Mrundi
mwenzake, Laudit Mavugo ya kushinda mtihani huo.
Pogba ambaye ni mchezaji ghali zaidi duniani, ameshindwa kuonyesha
thamani yake tangu ajiunge na Man United akitokea Juventus msimu huu,
huku sababu ikielezwa ni kutokana na kupania kuwafunga mdomo
wanaomkosoa.
Hata hivyo, Tambwe ambaye kwa sasa amelizoea soka la Bongo, anaiona
hali kama hiyo inaweza kumwaathiri Mavugo hivyo amemwambia siri pekee ya
kushinda mtihani huo ni kuweka pamba maskioni.
Tambwe ambaye pia kwa mara ya kwanza kutua nchini aliichezea Simba,
akizungumza na mwandishi wa habari hizi mapema wiki hii, alisema kelele
za mashabiki zinaweza kumpoteza Mavugo kabisa, hivyo anapaswa kuelekeza
akili mchezoni badala ya kuwasikiliza.
Alisema licha ya nyota huyo aliyeichezea Vital’O ya Burundi msimu
uliopita, kusajiliwa Simba kwa dau kubwa, katika mechi saba alizocheza
Ligi Kuu Tanzania Bara bado hajaonyesha kiwango chake anachokifahamu.
“Kama atachukua ushauri wangu, atakuwa mchezaji bora kwani ninajua
uwezo wake, tumekua pamoja kwenye kikosi cha timu ya taifa,” alisema
Tambwe.
“Nakumbuka nilivyokuja Simba nilicheza mechi nne bila kufunga bao,
Wabongo wakaanza kusema sina kiwango cha kuichezea timu hiyo, mara ya
kwanza nilianza kukata tamaa, ila nilipata ushauri kutoka kwa baadhi ya
wachezaji kwamba nikae mbali na maneno ya mashabiki pamoja na magazeti,
niliamua kucheza soka na kujiweka sawa kisaikolojia, ili nifanye
kilichonileta Tanzania.
DOWNLOAD
APP YETU YA SWAHIBA NEWS ILI UWEZE KUPATA HABARI ZOTE MOJA KWA MOJA
KUPITIA SIMU YAKO YA MKONONI BILA KUINGIA KWENYE WEBSITE,KUDOWNLOAD
BONYEZA HAPA
ANDIKA MAONI YAKO HAPO CHINI
Post A Comment: