MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imewataka wafanyabiashara
wenye leseni za kuingiza simu nchini, zinazotolewa na mamlaka hiyo,
kutekeleza maagizo yaliyotolewa na Kampuni ya Samsung ya kurejesha simu
za kisasa za Samsung Galaxy Note 7 baada ya kubainika zina matatizo ya
betri.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Meneja Mawasiliano wa
TCRA, Innocent Mungy, alisema ni vyema mawakala hao wakatekeleza maagizo
hayo, kwani simu hizo ni hatari kuendelea kutumika.
Aidha Mungy aliwataka wananchi ambao tayari wanatumia simu hizo
kuzizima na kuzirudisha haraka katika maduka walikozinunua ili kuepusha
hatari ambayo tayari Sumsung wameshaitoa.
“Simu hiyo tayari Samsung wenyewe wamesema ina matatizo ya betri na
mara mbili sasa imelipuka, hakuna faida ya mtu kuendelea kuitumia
unaweza ukasababisha hatari kubwa, inapolipuka inaweza kukuondoa mikono,
inaweza kulipua nyumba na matatizo mengine tunawataka wenye simu hizo
kuziridisha haraka,” alisema Mungy.
Pia alisema simu hiyo haijasambaa hapa nchini, lakini kuna watu
wanaweza kuwa wameletewa zawadi au mtu alisafiri na kuamua kuinunua.
“Taarifa tulizonazo haijaingia sana hapa nchini lakini wapo
walioletewa kama zawadi kutoka nje ya nchi nawaomba warudishe huko
kuepuka matatizo yanayoweza kujitokeza,” aliongeza Mungy.
Hivi karibuni Samsung ilitangaza kwamba haitaunda tena simu aina ya
Galaxy Note 7 baada ya kutokea kwa ripoti kwamba simu ambazo kampuni
hiyo iliamini ziko salama, zinawaka moto.
Kampuni hiyo ilikuwa tayari imepunguza uundaji wa simu hizo na
iliwataka waliokuwa na simu hizo, kuzizima na kuacha kuzitumia huku
uchunguzi ukiendelea.
Samsung iliwataka watu waliokuwa wamenunua jumla ya simu milioni 2.5
mwezi Septemba mwaka huu, kuzirejesha madukani baada ya wateja wengi
kulalamika kwamba betri za simu hizo zilikuwa zinalipuka.
Katika hatua
nyingine, wiki iliyopita, Kampuni hiyo ya Samsung ya Korea Kusini
ilitangaza kuwa imesitisha utengenezaji wa simu aina ya Galaxy Note 7.
DOWNLOAD
APP YETU YA SWAHIBA NEWS ILI UWEZE KUPATA HABARI ZOTE MOJA KWA MOJA
KUPITIA SIMU YAKO YA MKONONI BILA KUINGIA KWENYE WEBSITE,KUDOWNLOAD
BONYEZA HAPA
ANDIKA MAONI YAKO HAPO CHINI
Post A Comment: