WAKATI Tanzania leo ikiadhimisha kumbukumbu ya miaka 17 tangu
kufariki kwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Rais mstaafu wa
Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi amesema ana wasiwasi na Taifa la sasa
kwani halina uadilifu, aliotujengea Mwalimu Nyerere.
Mwinyi aliyerithi mikoba ya urais kutoka kwa Mwalimu Nyerere mwaka
1985, alisema hayo jana jijini Dar es Salaam alipokuwa akifungua mdahalo
wa kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere na kuzindua kitabu cha 'Selective
works of Mwalimu Nyerere', kilichotafsiriwa na wasomi kutoka China.
Mdahalo huo uliandaliwa na Taasisi ya Uongozi ikishirikiana na
Ubalozi wa China na Asasi ya Urafiki kati ya Tanzania na China. Mwalimu
Nyerere aliyeitawala Tanzania kwa takribani miaka 24, alifariki dunia
Oktoba 14, 1999 kwenye Hospitali ya St Thomas jijini London nchini
Uingereza ambako alikuwa akitibiwa maradhi ya saratani ya damu.
Aliiongoza Tanzania kwa uadilifu mkubwa akisimamia misingi ya haki,
umoja, mshikamano, kupiga vita rushwa, kusisitiza kujitegemea na
uzalendo kwa nchi.
“Kazi za kawaida kweli zinafanywa na zinaendelea, lakini sina uhakika
hata kidogo kama uadilifu aliotuachia Mwalimu bado tunao, sijui nani wa
kulaumiwa,” alisema Mwinyi maarufu kama Mzee Ruksa. Alisema kwa namna
ambavyo mambo yanakwenda, ni kiashiria tosha kuwa nchi haina uadilifu
tena.
“Mambo yanavyokwenda kama gari lililo katika usukani,” alieleza
Mwinyi na kuongeza kuwa kuna kila sababu ya kutafakari hali ilivyo sasa
ikilinganishwa na ile ambayo iliachwa na Baba wa Taifa miaka hiyo 17
toka kufa kwake.
Alisema nafasi hiyo ya mazungumzo katika mdahalo, inawapasa kukaa
kutafakari namna ya kurudisha nchi kwenye reli ambayo iliachwa na
Mwalimu Nyerere ambaye ndiye muasisi wa taifa hili katika misingi ya
uongozi.
“Tuna utajiri wa machoni, lakini ndiyo aliyokusudia Mwalimu?
Alitufundisha tuwe matajiri wa vitu au matajiri wa moyo? Tujali vitu au
tujali utu?" Alihoji Rais huyo mstaafu.
DOWNLOAD
APP YETU YA SWAHIBA NEWS ILI UWEZE KUPATA HABARI ZOTE MOJA KWA MOJA
KUPITIA SIMU YAKO YA MKONONI BILA KUINGIA KWENYE WEBSITE,KUDOWNLOAD
BONYEZA HAPA
ANDIKA MAONI YAKO HAPO CHINI
Post A Comment: