WAZIRI wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Charles Mwijage ametoa siku
nne kwa wafanyabiashara waliopitisha makontena 100 bandarini bila
kukaguliwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS), wakatoe taarifa katika
shirika.
Mwijage alitoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam jana wakati
akizungumza na waandishi wa habari baada ya kupata taarifa kuwepo kwa
makontena 100, yaliyotolewa bandarini kwa siku zilizopita bila
kukaguliwa na TBS.
“Nawataka wafanyabiashara wote waliochukua kontena hizo,
wajisalimishe haraka TBS kabla ya kufika Jumanne ili wakaguliwe. Najua
kuanzia kesho (leo) ni mapumziko, lakini TBS itaweka dawati la
kuwasikiliza mpaka Jumatatu na ikifika Jumanne hatua zitachukuliwa kwa
wahusika wote,” amesema Mwijage.
Alisema wafanyabiashara ambao hawatajisalimisha baada ya kumalizika
kwa siku hizo, hatua stahiki zitachukuliwa ikiwemo kulipa faini ya
asilimia 15.
Aidha, alisema kwa mawakala wa forodha wote, waliohusika kutoa
kontena hizo wizara yake itawasiliana na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk
Philip Mpango ili kuona hatua za kuchukua kwa kuwa serikali haiwezi
kukubali mchezo huo.
“Tayari tulishafunga michezo ya namna hii na tumeanza maisha mapya
kwa hiyo mawakala na wote mliohusika kutoa kontena hizo sababu
hazijafika mbali tunaomba mtueleze zilipo ili tukazikague,” aliongeza.
Pia alisema kontena hizo zilipaswa kukaguliwa na TBS, lakini baada ya
tukio hilo kontena hizo zitakaguliwa na shirika hilo wakishirikiana na
Tume ya Ushindani Tanzania (FCC). Aidha, amewaagiza TBS na FCC
wafuatilie watu wao na kuziona bidhaa hizo, kwani watakaoshindwa
hawatapewa cheti cha ubora bila kuona bidhaa na kukaguliwa.
DOWNLOAD
APP YETU YA SWAHIBA NEWS ILI UWEZE KUPATA HABARI ZOTE MOJA KWA MOJA
KUPITIA SIMU YAKO YA MKONONI BILA KUINGIA KWENYE WEBSITE,KUDOWNLOAD
BONYEZA HAPA
ANDIKA MAONI YAKO HAPO CHINI
Post A Comment: