MAALIM
Seif Sharif Hamad, Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), amewataka
Wazanzibari kusimama imara katika kulinda visiwa hivyo.
Amesema, mikakati inafanywa na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ili kuhakikisha maoni katika Katiba pendekezwa yanapita jambo ambalo litasababisha Zanzibar kupokwa mamlaka na kuzima ndoto za Wazanzibari.
Ameonesha hofu yake kutokana na Serikali ya CCM kutokuwa na dhamira ya kweli ya kuifanya Zanzibar kuwa na mamlaka kamili jambo ambalo Wazanzibari wamekuwa wakilipigania kwa muda mrefu.
Akizungumza na waumini wa Dini ya Kiislam baada ya Swala ya Ijumaa kwenye Msikiti wa Mbuyuni, Mkoa wa Mjini Magharibi visiwani humo Maalim Seif ambaye alikuwa Makamu wa Kwanza wa Rais katika Serikali ya Umoja wa Kitafa (SUKI) iliyopita amesema, Katiba inayopendekezwa inakwenda kumaliza kabisa ndoto ya Zanzibar kuwa mamlaka kamili na kwamba, wananchi wanapaswa kuungana na kupinga kwa nguvu zote.
Ametoleo mfano suala la ardhi ambalo ndani ya Katiba pendekezwa limewekwa kuwa la Jamhuri na kwamba, licha ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar (BLW) kupitisha sheria ya utafiti na uchimbaji madini na gesi, haitawezekana kwa kuwa ardhi ni suala la Muungano.
Maalim Seif amesema, kwa kuwa Serikali ya CCM inajua kuwa itakumbana na upinzani mkali wakati wa kura ya maoni, hivyo imeanza kusomba watu kutoka Bara kwenda visiwani ili kuongeza nguvu ya kuungwa mkono.
“Kwa kuwa Katiba hii inakuja kumaliza kabisa mamlaka ya Zanzibar, umeanza kufanyika mpango ili wapitishe kwa udanganyifu.
“Kuna watu wanatoka bara na kuletwa Zanzibar ili wapate sababu ya kupitisha na ionekane Wanzibari wameridhia,” amesema Maalim Seif.
Pamoja na kuwepo kwa mikakati hiyo kiongozi huyo wa CUF amesema kuwa, mbinu hizo hazitafanikiwa ila kwa sharti la Wanzanibari kusimama imara katika kuitetea Zanzibar.
DOWNLOAD
APP YETU YA SWAHIBA NEWS ILI UWEZE KUPATA HABARI ZOTE MOJA KWA MOJA
KUPITIA SIMU YAKO YA MKONONI BILA KUINGIA KWENYE WEBSITE,KUDOWNLOAD
BONYEZA HAPA
ANDIKA MAONI YAKO HAPO CHINI
Post A Comment: