Rais John Magufuli amempa miezi miwili mtoto wa dada yake, ambaye ni
Meneja wa Shirika la Umeme (Tanesco) mkoa wa Pwani, Mhandisi Martin
Madulu, kuhakikisha umeme unafika kwenye kiwanda cha kusindika matunda
cha kampuni ya Bakhresa kilichomo ndani ya mkoa wake, vinginevyo
atamtumbua.
Rais alitoa agizo hilo wakati wa uzinduzi wa kiwanda hicho kilichopo Vikindu wilayani Mkuranga mkoani humo, agizo ambalo limekumbusha jinsi alivyomtumbua aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga aliyekuwa anadaiwa kuwa rafiki yake wa karibu.
Uteuzi wa Kitwanga kwenye Baraza la Mawaziri ulitenguliwa na Magufuli Mei 20, mwaka huu baada ya Mbunge huyo wa Misungwi (CCM) kuingia bungeni akiwa amelewa na kujibu swali lililoelekezwa kwenye wizara yake.
Na katika uzinduzi wa kiwanda hicho jana, Rais ambaye alikuwa mgeni rasmi, alilazimika kutoa agizo hilo kwa mpwa wake mara tu baada ya kuelezwa na mmoja wa wakurugenzi wa kampuni hiyo, Aboubakar Bakhresa, kuwa wanalazimika kutumia jenereta kukiendesha kutokana na kutokuwapo kwa nishati ya umeme wa Tanesco.
Aboubakar alimweleza Rais kuwa upatikanaji wa umeme bado ni changamoto katika kiwanda hicho na kwamba wanahitaji umeme wa megawati 10 ili kukiendesha.
“Meneja wa Tanesco mkoa wa Pwani, wewe Madulu, tena ni mtoto wa dada yangu, nitakutumbua wewe!" Alisema Rais Magufuli na kufanya umati uliohudhuria halfa hiyo uangue kicheko.
"Ulifanya kazi nzuri ulipokuwa Kagera na Tanga, sasa fanya kazi na hapa. "Nataka ndani ya miezi miwili umeme uwe umefika hapa, mimi huwa sibembelezi mtu, mkono wangu ni mwepesi sana kutumbua.”
DOWNLOAD
APP YETU YA SWAHIBA NEWS ILI UWEZE KUPATA HABARI ZOTE MOJA KWA MOJA
KUPITIA SIMU YAKO YA MKONONI BILA KUINGIA KWENYE WEBSITE,KUDOWNLOAD
BONYEZA HAPA
ANDIKA MAONI YAKO HAPO CHINI
Post A Comment: