Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo
tarehe 14 Oktoba, 2016 amekutana na kufanya mazungumzo na Naibu Waziri
wa Biashara wa Jamhuri ya Watu wa China Mhe.Qian Keming
Katika mazungumzo hayo, viongozi hao wamekubaliana kuharakisha miradi
inayotekelezwa kwa ushirikiano wa nchi hizo mbili ukiwemo mradi wa
ujenzi wa reli ya kati.
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam Rais
Magufuli amemueleza Mhe. Qian Keming kuwa Serikali yake ya awamu ya tano
inataka kuona mambo yakifanyika na kutoa matokeo bila kupoteza muda na
kwamba angependa wadau wa maendeleo hasa nchi ya China ambayo ni ndugu
na rafiki mkubwa wa Tanzania iende katika kasi hiyo hiyo.
Rais Magufuli ameuzungumzia mradi wa ujenzi wa reli ya kati ya kutoka
Dar es Salaam, Mwanza, Kigoma na kuunganisha nchi za Rwanda na Burundi
ambao Tanzania imetenga Shilingi Trilioni moja kwa ajili ya kuanza
ujenzi katika bajeti hii, kwa kutaka China ambayo imekubali kushiriki
katika ujenzi iendane na kasi ya Serikali yake.
“Mhe. Qian Keming sisi tumeamua kuanza ujenzi na tayari Wakandarasi
32 wamejitokeza kuomba kujenga reli ya kati kuanzia Dar es Salaam hadi
Morogoro umbali wa kilometa 200 za mwanzo na tutatumia fedha zetu
wenyewe.
“Kazi hii tunataka ianze mwaka huu wa fedha, kwa sababu upembuzi
yakinifu na usanifu umeshafanyika, kwa hiyo na nyie ongezeni kasi ili
mradi huu wote ukamilike, nataka uwe umekamilika kabla sijaondoka
madarakani” amesema Rais Magufuli.
Dkt. Magufuli ameongeza kuwa mradi huo una manufaa makubwa kwa
Tanzania na nchi nyingine nane zinazotegemea bandari ya Dar es Salaam na
kwamba kukamilika kwake kutatoa mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi
wa Tanzania ambayo imedharia kuwa nchi ya kipato cha kati ifikapo mwaka
2025.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Biashara wa China Mheshimiwa Qian
Keming amempongeza Rais Magufuli kwa kazi kubwa anayoifanya ya kukuza
uchumi wa Tanzania, kupiga vita rushwa na kwa namna ya kipekee kwa
dhamira yake ya kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano na China na
ameahidi kuwa Serikali ya China itaongeza msukumo katika uharakishaji wa
utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa reli ya kati.
“Mheshimiwa Rais Magufuli nimeielewa dhamira yako na kiu uliyonayo,
naona kabisa kwamba dhamira ya kisiasa ipo ya kutosha, tunachotakiwa
kukifanya ni kuwasukuma wataalamu wetu waongeze kasi, na mimi nakuahidi
kuwa tulikuwa tunakwenda kwa kasi ya kilometa 100 kwa saa, sasa
tutaongeza na kwenda kilometa 200 kwa saa” amesema Mhe. Qian Keming.
DOWNLOAD
APP YETU YA SWAHIBA NEWS ILI UWEZE KUPATA HABARI ZOTE MOJA KWA MOJA
KUPITIA SIMU YAKO YA MKONONI BILA KUINGIA KWENYE WEBSITE,KUDOWNLOAD
BONYEZA HAPA
ANDIKA MAONI YAKO HAPO CHINI
Post A Comment: