SAKATA la kupanda kwa bei ya sukari limeibuka tena bungeni na safari
hii Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM) ameomba mwongozo wa
kutaka Kikao cha Bunge kiahirishwe ili kujadili suala hilo la dharura.
Akitumia kifungu cha Kanuni za Bunge cha 47(1, 2, 3), mbunge huyo
alisema bungeni mjini hapa jana, kuwa suala hilo ni muhimu kwa
Watanzania hivyo ni vyema likajadiliwa na kupatiwa ufumbuzi haraka
iwezekanavyo.
Alisema tangu itangazwe utaratibu wa kusitisha sukari kuingizwa
nchini kutoka nje, bidhaa hiyo imekuwa adimu na bei yake imekuwa
inapanda kila siku na kusababisha maisha ya wananchi kuzidi kuwa magumu.
Hata hivyo, kabla ya kumaliza kuwasilisha hoja yake hiyo, Naibu Spika
wa Bunge, Dk Tulia Ackson alimkatisha na kubainisha kuwa hoja hiyo si
dharura, lakini pia tayari ilishatolewa ufafanuzi na Waziri Mkuu, Kassim
Majaliwa.
Wiki iliyopita, Waziri Mkuu akijibu hoja iliyoibuliwa bungeni hapo
inayohusu pia bei ya sukari, Waziri Mkuu alisema serikali imeruhusu
kiasi kidogo cha sukari kuingizwa nchini ili kupunguza tatizo la
upungufu wa bidhaa hiyo.
Kwa mujibu wa Majaliwa, Tanzania ina uwezo wa kuzalisha tani 300,000
za sukari kwa mwaka wakati nchi inahitaji tani 420,000 hivyo kuwepo na
upungufu wa tani 120,000.
DOWNLOAD
APP YETU YA SWAHIBA NEWS ILI UWEZE KUPATA HABARI ZOTE MOJA KWA MOJA
KUPITIA SIMU YAKO YA MKONONI BILA KUINGIA KWENYE WEBSITE,KUDOWNLOAD
BONYEZA HAPA
Post A Comment: