Katika kukabiliana na maradhi ya kipindupindu yaliyodumu kwa zaidi ya
miezi saba na kusababisha vifo vya watu 57 huko visiwani Zanzibar, Nchi
wahisani zinaendelea kutoa misaada ya madawa pamoja na ya kibinadamu,
kwa lengo la kuiunga mkono Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika
kukabiliana na maradhi hayo.
Balozi wa Kuwait hapa nchini, Bwana Jasem Al Najem ametembelea kambi
ya wagonjwa wa kipindupindu iliyopo katika eneo la Chumbuni na kupatiwa
maelezo na Daktari dhamana wa kanda ya Unguja Dk Fadhil Mohamed ambaye
amemuwakilisha Waziri wa Afya Mahmoud Thabit Kombo.
Balozi Jasem amesema mbali na msaada huo wa awali, ameitaka mamlaka
inayohusika kuwapatia orodha ya mahitaji muhimu ikiwemo madawa, vifaa
vya matibabu pamoja na maji vitakavyotolewa mara moja ili kuongeza nguvu
za kukabiliana na maradhi hayo yanayokatisha uhai wa maisha ya wananchi
wa visiwa vya Unguja na Pemba.
Kwa upande wake, Dk.Fadhil Mohamed amesema hatua mbalimbali
zimechukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa lengo la
kukabiliana na maradhi hayo, ikiwemo kupiga marufuku uuzwaji wa vyakula
katika migahawa pamoja na kutoa elimu kwa umma namna ya kujikinga na
mardhi hayo na matumizi bora ya maji safi na salama.
Post A Comment: