Aidha, Jaji Warioba ameendelea ‘kuililia’ rasimu ya Katiba
iliyotayarishwa na iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba aliyokuwa
akiiongoza, akieleza maeneo muhimu yanayopaswa kuwapo katika Katiba
inayopendekezwa kabla ya kupigiwa kura ya maoni.
Pia, amebainisha kasoro kadhaa zilizojitokea katika uchaguzi mkuu
mwaka jana, ambazo amesema zisipofanyiwa kazi taifa litaendelea
kudidimia na kushindwa kuimarisha demokrasia.
Jaji Warioba alisema hayo jijini Dar es Salam jana, wakati
akizungumza katika mkutano wa kitaifa wa tathimini ya uchaguzi mkuu wa
mwaka jana ulioandaliwa na Mpango wa Utafiti na Elimu ya Demokrasia
Tanzania (Redet) kwa kushirikiana na Kituo cha Sheria na Haki za
Binadamu (LHRC).
Warioba ambaye alikuwa Waziri Mkuu enzi za Mwalimu Nyerere, mbali na
kutaja maeneo tisa ambayo anataka yaangaliwe katika Katiba pendekezwa
iliyoandaliwa na Bunge Maalum la Katiba kabla ya hatua ya kura ya maoni
endapo Tanzania inataka kujipambanua kuwa na demokrasia bora.
Hata hivyo, Jaji Warioba alisifia uchaguzi mkuu uliopita kuwa ulikuwa
huru na haki pamoja na mamlaka husika kuwajibika kutoa hamasa kwa
wapigakura.
Mambo tisa aliyoainisha akitaka yapewe nafasi katika Katiba pendekezwa ni:-
KURA ZA RAIS, KUHOJI MATOKEO
Jaji Warioba alisema kwa mujibu wa Katiba, Rais anachaguliwa kwa
wingi wa kura hata kama hazikufika nusu ya wapigakura na Tume ya Taifa
ya Uchaguzi (Nec) ikishatangaza hakuna anayeruhusiwa kuhoji kokote.
“Haya ni mambo yanayozungumziwa na kulalamikiwa kwa muda mrefu, Rais
ni wa taifa hata kama anatokana na chama cha siasa ni vizuri achaguliwe
na wengi na siyo wingi wa kura. Ni vizuri apate zaidi ya nusu na
iruhusiwe kuhoji matokeo. Katiba mpya ndiyo itakayoondoa vikwazo hivi,”
alisema.
Jaji Warioba ambaye alikuwa mchokoza mada, alisema muundo wa sasa
hausaidii vyama vidogo, bali kuvibeba vikubwa ilhali wanawakilisha kundi
kubwa kuliko la waliopiga kura.
VITI MAALUM
Alisema mapendekezo yao ni kupatikana kwake kuwe kwa uwiano na kusiwe
na makadirio ya theluthi moja ili kuondoa kuwa wa daraja la chini na
kukosa nguvu ya moja kwa moja kwa wananchi.
“Madhara ni kuwa na Bunge kubwa kila mwaka, tunaogopa nini kwenda kwenye kura ya uwiano?” alihoji.
Kwa upande wa Zainzibar, alisema Katiba yao imeeleza kuwa chama
kitakachopata asilimia 10 kinakuwa sehemu ya serikali na kwamba kuna
umuhimu wa kura ya uwiano ili vyama vidogo, wanawake na makundi mengine
yawakilishwe vyema.
Alisema kikwazo kingine kwa viti maalum ni kutengwa kikatiba, kama kutokuwa waziri mkuu.
TUME HURU YA UCHAGUZI
Jaji Warioba alisema licha ya Nec kufanya vizuri katika uchaguzi wa
mwaka jana, lakini baadhi ya wadau wa uchaguzi hawana imani na tume hiyo
na wana malalamiko mengi.
"Lazima tufanye namna ya kuifanya iaminike kwa wadau wote. Ndiyo
maana kwenye rasimu ya wananchi tulipendekeza kuwe na kamati maalum,
mwenyekiti wake awe Jaji Mkuu itakayopeleka majina kwa Rais kwa ajili ya
kuteua na majina ya wajumbe yapelekwe bungeni kwa uthibitisho,”
alisema.
Kuhusu watumishi wa tume mikoani wanaotumika watumishi wa umma ambao
mara kwa mara wamelalamikiwa kuharibu uchaguzi, alisema rasimu
ilipendekeza kuwapo kwa wasimamizi wa kanda watakaowajibika katika eneo
husika ambao watakuwa watumishi wa Nec.
GHARAMA ZA UCHAGUZI
Alisema sheria ya uchaguzi ipo lakini haiwezi kutekelezwa kwa kuwa
vyama vikubwa vina nafasi ya kupata fedha nyingi kuliko vidogo.
“Uchaguzi wa mwaka jana waliweka fedha mbele, moja ya kitu
kinachoumiza uchaguzi ni matumizi makubwa ya fedha. Uchaguzi umekuwa
biashara, wanaotafuta nafasi kwa kununua ni lazima waangaliwe.
TUME HAKI ZA BINADAMU
Alisema katika rasimu walipendekeza kuwapo kwa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, lakini Bunge lilitupa.
“Tuanze kujenga misingi tuwe na tume za kitaifa. Cha kwanza ni utu ukishasema binadamu wote ni sawa hutawabagua, mtaona wote ni sawa, uwazi na uwajibikaji.”
TUME YA MAADILI
Alisema wakati wa mchakato wa mabadiliko ya Katiba walipokea maoni ya
wananchi mengi yakizungumzia maadili yameporomoka sana ndani ya jamii
na kwa viongozi.
“Tuliona haitoshi tukaona tuweke misingi na miiko ya uongozi na kuwe
na utaratibu wa kusimamia na tulisema kuwe na tume yenye madaraka badala
ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora isimamie haki za binadamu.
Ya Uwajibikaji iwe na tume ya maadili na siyo sekretarieti iliyopo sasa
,” alisema na kuongeza:
“Kama kuna kitu kimeniumiza sana kwenye rasimu ni kuondoa hili (Tume
ya Maadili), yaani ilivyovurugwa nilikuwa nashangaa sana na kusema
uzalendo ni sifa ya uongozi ya utawala bora, uzalendo unataka mtu mwenye
utawala bora, ni hazina. Hili tulifanyie kazi tutahangaika sana
tusipokuwa na utamaduni huu ni bure,” alisema.
RUSHWA
Jaji Warioba alisema bado kuna kazi kubwa ya kufanya ndani na nje ya
vyama kwani matatizo ya rushwa yanaanzia kwenye vyama, viongozi kutumia
madaraka yao vibaya, viongozi kuwa wepesi kuinyooshea Nec vidole na
kutaka ibadilishe badhi ya mambo ambayo ndani ya vyama vyao wameshindwa
kuyafanya.
Alisema kukiwa na vyama ambavyo havina demokrasia hukuwezi kuwa na
uchaguzi wa kidemokrasia, hivyo ni lazima kupiga kelele kuhakikisha
demokrasia inakuwapo.
MUUNGANO
Aidha, Jaji Warioba ambaye hakueleza kwa undani suala hilo, alisema
mambo ambayo Mwalimu Nyerere aliyawekea mkazo mkubwa ni kupinga rushwa
na ufa katika Muungano ambao ni lazima ushughulikiwe na kwamba ni moja
ya mambo ya msisitizo kwenye Katiba.
MGOMBEA HURU
Alisema wakati wa mchakato wa maoni ya wananchi, wengi walitaka
kuwapo kwa mgombea binafsi na kuondokana na utaratibu wa vyama pekee
kuwa na nguvu, lakini Bunge Malum liliweka mapendekezo hayo na masharti
magumu katika sheria ngumu ambayo haiwezi kubadilishwa kwa haraka huku
wagombea wengine wakiongozwa na sheria ya uchaguzi.
“Uchaguzi ulikwenda vizuri, lakini kuna mambo yalijitokeza ambayo
lazima tuyaboreshe ili tuendako uwe mzuri zaidi wa haki zaidi na
kuimarisha demokrasia. Katika mchakato wa Katiba mpya kuna mambo ya
jumla ambayo lazima yaangaliwe vinginevyo yataleta matizo makubwa katika
nchi,” alisema.
AMFAGILIA MAGUFULI
Mbali na kuelezea mambo hayo, pia Jaji Warioba aliisifu serikali ya
awamu ya tano nayoongozwa na Rais Jaohn Magufuli kuwa mwanzo wake ni
mzuri kwani imeweka msisitizo katika maadili , uadilifu, kubana
matumizi, kupiga vita rushwa, kupeleka fedha mahali wananchi watanufaika
na kupiga vita ufisadi.
Alisema mwenendo huo unapaswa kuwa mwitikio nchi nzima pamoja na kuangalia namna ya kuwa sehemu ya Katiba.
KSORO CHA UCHAGUZI 2015
Alisema katika uchaguzi wa mwaka jana lugha za kejeli, matusi na
kebehi vilitawal, huku vyombo vya habari vikitumika na kutia doa na
kwamba umeacha majeraha makubwa kwani kwenye siasa lugha za kupingana
kwa hoja zinakubalika ila za kujeruhi moyo ni ngumu kutibu.
Alisema lugha mbaya inaleta uhasama kati ya wananchi na kwamba lugha
iliyotumika katika uchaguzi huo imeacha makovu na kwamba sasa viongozi
waliotumia lugha hizo dhidi ya wengine wanashindwa kusalimianana, hivyo
ni vyema kukosoa kwa ustaarabu.
Jingine ni ubaguzi wa dini, ukabila, uvyama na ukanda ambavyo
vinaendelea hadi sasa kwenye mitandao ya kijamii, hivyo visipo
shughulikiwa taifa litafika pabaya.
VYOMBO VYA HABARI
Jaji Warioba alisema hakuna chombo cha habari ambacho hakikuonyesha
upande kisiasa, huku baadhi vikiwa na ushabiki wa wazi na kwamba
waliotoa tathimini ya utendaji wa vyombo vya habari wakati wa uchaguzi
walijikita katika idadi ya habari tuna si maudhui.
DOWNLOAD
APP YETU YA SWAHIBA NEWS ILI UWEZE KUPATA HABARI ZOTE MOJA KWA MOJA
KUPITIA SIMU YAKO YA MKONONI BILA KUINGIA KWENYE WEBSITE,KUDOWNLOAD
BONYEZA HAPA
Post A Comment: