KIKOSI CHA SAGRADA ESPERANCE |
SIKU moja baada ya kutolewa na Al Ahly ya Misri katika hatua ya 16
Bora ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga imeangukia kwa Sagrada Esperanca
ya Angola katika michuano ya kuwania ubingwa wa Kombe la Shirikisho
Afrika.
Itakutana na Waangola hao katika hatua ya mtoano ambayo mshindi wake
ataingia hatua ya makundi ya michuano hiyo inayoshika nafasi ya pili kwa
ukubwa katika ngazi za klabu barani Afrika.
Kwa mujibu wa ratiba iliyopangwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF)
jana alasiri, Yanga baada ya kufungwa 2-1 na Ahly juzi usiku huko
Alexandria na hivyo kutolewa kwa jumla ya mabao 3-2, sasa itakipiga
dhidi ya timu hiyo inayomilikiwa na Shirika la Madini la Taifa la
Angola.
Itaanza kwa kuwakaribisha Waangola hao kati ya Mei 6 na 8 jijini Dar
es Salaam na marudiano kuwa kati ya Mei 17 na 18 nchini Angola.
Haijafahamika Angola zitachuana katika mji gani, ingawa Sagrada
iliyoanzishwa Desemba 22, mwaka 1976, yaani miaka 39 iliyopita, uwanja
wake wa nyumbani upo Dundo, katika Jimbo la Lund Norte ambao una uwezo
wa kuingiza mashabiki 3,000 kwa wakati mmoja.
Endapo itafanikiwa kuwang’oa Sagrada inayonolewa na Zoran Mackic,
raia wa Serbia, Yanga itakuwa imejihakikishia kusaka mamilioni ya fedha
katika michuano hiyo ambayo mshindi wake hutwaa kitita cha dola za
Kimarekani 625,000 (Sh bilioni 1.36).
Mshindi wa pili hupata dola 432,000 (Sh milioni 907) wakati timu
zinazoshika nafasi ya pili na ya tatu katika kila kundi hupata dola
239,000 (Sh milioni 500) na ya mwisho katika kundi, yaani inayoshika
nafasi ya nne, huambulia dola 150,000 (Sh milioni 315).
DOWNLOAD
APP YETU YA SWAHIBA NEWS ILI UWEZE KUPATA HABARI ZOTE MOJA KWA MOJA
KUPITIA SIMU YAKO YA MKONONI BILA KUINGIA KWENYE WEBSITE,KUDOWNLOAD
BONYEZA HAPA
Post A Comment: