MAMLAKA ya Chakula na Dawa nchini (TFDA) imeifunga machinjio ya nyama
ya mjini Tabora kwa muda usiojulikana, baada ya kushindwa kutekeleza
makubaliano ya kuondoa uchafu na kukarabati mifumo ya maji safi na maji
taka ili kunusuru afya za walaji.
Kaimu Meneja wa mamlaka hiyo Kanda ya Magharibi, Dk Edgar Mahundi
alisema wamefikia hatua hiyo baada ya uongozi wa Halmashauri ya Manispaa
ya Tabora pamoja na mambo mengine kushindwa kufanya usafi kama
walivyoagiza siku saba zilizopita.
Alisema TFDA iliipa manispaa hiyo wiki moja iwe imekarabati mifumo ya
maji safi na maji taka pamoja na kuondoa uchafu uliokuwa umerundikana
katika maeneo ya machinjio hayo.
Dk Mahundi alibainisha kuwa uongozi wa Halmashauri ya manispaa ya
Tabora ulichokifanya ni kuweka bomba la maji na kupima afya za watumishi
wa machinjio hiyo pasipo kufanya usafi wa eneo linalozunguka machinjio
hiyo.
Aliyataja baadhi ya mambo ambayo hayakutekelezwa ni pamoja na
kuchimba shimo la maji taka, eneo la kutupia kinyesi cha ng’ombe baada
ya kuchinjwa , ukarabati wa jengo la banda la kuhifadhia ngozi pamoja na
jengo linalotumika kuhifadhia mifugo kabla ya kuchinjwa.
Aidha Dk Mahundi amebainisha kuwa mamlaka hiyo iliagiza ujengwe uzio
wa machinjio hiyo ambao umechakaa ikiwa ni pamoja na kuweka lango kuu
moja ili kuzuia wizi wa mifugo.
Post A Comment: