WAZIRI wa Biashara na Viwanda wa Singapore, Dk Koh Poh Koon amesema
wamepanga kutumia Bandari ya Dar es Salaam kuwa kiunganishi cha biashara
kati ya nchi hiyo na mataifa mengine ya Afrika Mashariki (EAC).
Dk Koon aliyasema hayo jana wakati alipomtembelea Waziri Mkuu, Kassim
Majaliwa ofisini kwake mjini Dodoma, na kwamba Singapore ipo tayari
kutoa fursa kwa wataalamu wa Tanzania kwenda kufanya kazi katika Bandari
ya Singapore ili kupata uzoefu utakaosaidia uendeshaji wa bandari za
Tanzania.
Dk Koon ambaye ameambatana na wafanyabiashara wakubwa wapatao 40,
alimweleza Waziri Mkuu kwamba Kampuni ya Hyflux ya Singapore, imeanza
kuwekeza nchini kwa kujenga eneo maalumu la uchumi mkoani Morogoro,
ambako ndani ya kipindi cha miaka mitano wanatarajia kujenga miundombinu
wezeshi ya kuweka viwanda vya kati, maeneo ya biashara na nyumba za
makazi zipatazo 37,000.
“Jiwe la msingi la mradi huo litawekwa tarehe 29 Aprili 2016 na
Waziri wa Biashara, Viwanda na Uwekezaji, Charles Mwijage,” alisema
waziri huyo wa Singapore.
Mbali na ushirikiano katika sekta ya biashara na uwekezaji, Dk Koon
alimweleza Waziri Mkuu kwamba nchi yake itaisaidia Tanzania kujenga
uwezo wa kiufundi katika maeneo mbalimbali ya menejimenti na uendeshaji
wa bandari na ufundi katika sekta ya gesi na mafuta.
“Hadi sasa makampuni ya Singapore yaliyowekeza nchini ni pamoja na
Pavillion Energy ambayo imewekeza kiasi cha Dola za Marekani bilioni 1.2
katika sekta ya gesi na inatarajia kuwekeza zaidi dola za kimarekani
bilioni tatu kwa ajili ya ujenzi wa kinu cha kuchakata gesi (LNG plant)
kitakachojengwa mikoa ya Kusini kwa ubia na makampuni ya gesi kutoka
Ulaya na Marekani,” alifafanua.
DOWNLOAD
APP YETU YA SWAHIBA NEWS ILI UWEZE KUPATA HABARI ZOTE MOJA KWA MOJA
KUPITIA SIMU YAKO YA MKONONI BILA KUINGIA KWENYE WEBSITE,KUDOWNLOAD
BONYEZA HAPA
Post A Comment: