WAKATI Rais John Magufuli akisisitiza kuwa utumbuaji majipu
utaendelea kufanyika hadharani bila kificho, pigo jingine kwa
waliotumbuliwa na wanaosubiri kutumbuliwa, limetangazwa.
Akisoma Mwelekeo wa Kazi za Serikali bungeni Waziri Mkuu,
Kassim Majaliwa, mbali na kusisitiza kuendelea kushughulikia watendaji
wazembe, wabadhirifu na wavivu, alitangaza kuwa Divisheni ya Mahakama ya
Rushwa na Ufisadi imeanzishwa katika Mahakama Kuu na itaanza kazi zake
Julai mwaka huu.
Hatua hiyo ni pigo kwa watuhumiwa wa ufisadi ambao tangu Serikali ya
Awamu ya Tano ilipoingia madarakani, wamekuwa wakichukuliwa hatua
hadharani ya kusimamishwa kazi kupisha uchunguzi dhidi ya tuhuma zao,
kiasi cha baadhi ya wanasiasa kushindwa kuvumilia na kujitokeza
kulalamika.
Miongoni mwa wanasiasa waliojitokeza kulalamikia hatua ya watuhumiwa
hao kuchukuliwa hatua ni Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema), Freeman Mbowe na aliyekuwa mgombea urais wa chama hicho
katika Uchaguzi Mkuu uliopita, Edward Lowassa.
Mahakama ya Rushwa
Mahakama hiyo ni moja ya ahadi zilizonadiwa na Dk Magufuli katika
Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2015-2020 wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu
mwaka jana, akisema katika Hotuba ya Ufunguzi wa Bunge na kuirejea
wakati wa uzinduzi wa Mwaka wa Mahakama na Siku ya Sheria Duniani.
Akitangaza kukamilika kwa mchakato huo jana, Waziri Mkuu Majaliwa
alisema: “Napenda kuliarifu Bunge kwamba Serikali imeanzisha Divisheni
ya Mahakama ya Rushwa na Ufisadi katika Mahakama Kuu itakayoanza kufanya
kazi Julai, 2016.”
Uharaka wa kesi
Mbali na kuanza kufanya kazi kwa mahakama hiyo, Waziri Mkuu Majaliwa
pia alisema kuwa Serikali itaimarisha Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka
(DPP) na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), ili ziharakishe
utoaji wa haki.
Uimarishwaji wa ofisi hizo pia unatokana na agizo la Rais Magufuli
alilotoa siku hiyo ya uzinduzi wa Mwaka wa Mahakama na Siku ya Sheria
Duniani, alipotaka kesi za uhujumu uchumi na ufisadi ziendeshwe kwa
kasi, ili jitihada za Serikali za kupambana na matatizo hayo, zizae
matunda.
Katika hotuba hiyo ya Siku ya Sheria Duniani, Rais Magufuli alielezea
kushangazwa na kitendo cha ofisi ya DPP, kuchelewa kuwapeleka
mahakamani watuhumiwa waliokamatwa na ushahidi.
Katika hotuba hiyo ya Majaliwa, iliyokwenda sambamba na makadirio ya
bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2016/17, alisema
Serikali itaendelea kuwawajibisha wale wote ambao hawataendana na
Falsafa na Mwelekeo wa Serikali ya Awamu ya Tano, lakini akasisitiza
kwamba serikali itachukua hatua kwa kuzingatia na kufuata Sheria, Kanuni
na Taratibu za Utumishi wa Umma.
“Ili yawepo mapinduzi ya kweli ya kuelekea kwenye uchumi wa Kati
tunaodhamiria ni lazima tuimarishe uwajibikaji na maadili kwa viongozi,
watendaji na kwa kila Mtanzania. Sote tumeshuhudia hatua zinazochukuliwa
na serikali dhidi ya watumishi wasio waadilifu, wanaotumia fedha za
umma na madaraka yao vibaya. “Ndio maana tumeanza kwa nguvu kuimarisha
nidhamu, uwajibikaji na matumizi sahihi ya fedha za umma ili zielekezwe
kwenye shughuli zenye manufaa kwa Watanzania walio wengi na si
vinginevyo,” alisema Waziri Mkuu Majaliwa.
Akizungumzia utekelezaji wa Sera ya Utoaji Elimu Bure kuanzia Darasa
la Kwanza hadi Kidato cha Nne, Waziri Mkuu Majaliwa alisema ipo
changamoto ya upungufu mkubwa wa madawati baada ya kuanza kuandikisha
watoto shule bila malipo.
Kutokana na hilo, aliwaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini
waliokamata mbao kutokana na makosa mbalimbali kutozipiga mnada mbao
hizo na badala yake watumie mbao hizo kutengeneza madawati kuanzia jana
na pia halmashauri kutumia rasilimali zake kutengeneza madawati kwa kila
shule.
DOWNLOAD
APP YETU YA SWAHIBA NEWS ILI UWEZE KUPATA HABARI ZOTE MOJA KWA MOJA
KUPITIA SIMU YAKO YA MKONONI BILA KUINGIA KWENYE WEBSITE,KUDOWNLOAD
BONYEZA HAPA
Post A Comment: