BAADA ya kuangukia katika michuano ya Kombe la Shirikisho ilikopangwa
kukutana na Sagrada Esperanca ya Angola katika hatua ya mtoano, kocha
wa Yanga, Hans van der Pluijm ameahidi makubwa.
Amesema anaamini timu yake ina nafasi kubwa ya kutinga hatua ya
makundi, hivyo atafanya kila linalowezekana kuhakikisha dhamira yake
inatimia, huku akitamba ana kikosi imara, isipokuwa kilikosa bahati
mbele ya Al Ahly ya Misri, katikati ya wiki hii.
Usiku wa Jumatano iliyopita, Yanga ilitolewa kwa jumla ya mabao 3-2
na Al Ahly kwenye mchezo wa raundi ya pili wa Ligi ya Mabingwa Afrika,
baada ya kukubali kipigo cha mabao 2-1, kwenye mchezo wa marudiano
kwenye Uwanja wa Borg El Arab, jijini Alexandria, Misri.
Pluijm alisema matumaini hayo yanatokana
na ari na ubora iliyokuwa nao kikosi chake ambacho kilipambana kufa
kupona katika mchezo na Al Ahly, licha ya kutolewa kwenye michuano hiyo.
“Siwezi kuwadharau wapinzani wetu Esperanca, lakini naamini
hawatakuwa bora kama ilivyokuwa kwa Al Ahly na kama hivyo, ndivyo basi
kuna uwezekano mkubwa wa Yanga kucheza hatua ya makundi kwa sababu tupo
kwenye kiwango bora hivi sasa,” alisema kocha huyo raia wa Uholanzi,
lakini mwenye uzoefu mkubwa na soka ya Afrika.
Esperanca inayomilikiwa na Shirika la Taifa la Madini la Angola, ina
nyota kadhaa akiwemo `babu’ mwenye umri wa miaka 37, lakini mwenye
makali ya upachikaji mabao, Arsenio Sebastiao Cabungula maarufu kama
Love ambaye mwaka 2006 alikuwa miongoni mwa nyota wa Angola waliocheza
Kombe la Dunia nchini Ujerumani.
DOWNLOAD
APP YETU YA SWAHIBA NEWS ILI UWEZE KUPATA HABARI ZOTE MOJA KWA MOJA
KUPITIA SIMU YAKO YA MKONONI BILA KUINGIA KWENYE WEBSITE,KUDOWNLOAD
BONYEZA HAPA
Post A Comment: