DK. Vincent Mashinji Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (chadema), amesema kuwa Katiba Mpya inayotokana na maoni ya wananchi ndiyo msingi imara pekee unaoweza kuweka mifumo na taasisi kwa ajili ya maendeleo ya kweli yatakayogusa maslahi ya Watanzania wote badala ya nchi kuongozwa na kauli za viongozi,
Kutokana na umuhimu huo wa kuzingatia maoni ya wananchi yanayobeba matakwa yao katika mchakato wa Katiba Mpya, amesema kuwa Chadema hakitashiriki kura ya maoni ya Katiba Mpya Inayopendekezwa ambayo ilipitishwa na Bunge Maalum la Katiba baada ya kubadili na kuondoa mapendekezo yaliyotolewa na wananchi kwenye Rasimu ya Pili ya Katiba Mpya.
Badala yake, Chadema kitaendelea kuweka agenda ya kupigania Katiba Mpya na bora katika vipaumbele vyake, kwa sababu itatibu vidonda na kumaliza makovu yaliyoko katika jamii kutokana na matatizo mbalimbali kama vile ukosefu wa haki, migogoro ya ardhi, wananchi kukosa huduma za msingi za kijamii zikiwemo elimu, maji na afya.
Dkt. Mashinji ameyasema hayo jijini Dar es Salaam alipoukaribisha ujumbe wa Chama cha Centre Party cha Norway uliofika ofisini kwake jijini Dar es Salaam kutia saini makubaliano ya ushirikiano kati ya vyama hivyo kwenye Mradi wa Elimu ya Demokrasia awamu ya pili unaofanyika Wilaya ya Mtwara Vijijini.
Dkt. Mashinji pia amekishukuru chama hicho kwa kusaidia kutoa elimu ya uraia kwa Watanzania hususani maeneo ya vijijini katika mradi ambao unahusisha vyama vyote vya siasa vyenye uwakilishi ndani ya Bunge, huku akisisitiza kuwa Chadema kiko tayari kwa ushirikiano unaozingatia maslahi na matakwa ya wananchi hasa katika kukuza uelewa wa kudai haki, demokrasia na uongozi bora ndani ya nchi.
DOWNLOAD
APP YETU YA SWAHIBA NEWS ILI UWEZE KUPATA HABARI ZOTE MOJA KWA MOJA
KUPITIA SIMU YAKO YA MKONONI BILA KUINGIA KWENYE WEBSITE,KUDOWNLOAD
BONYEZA HAPA
Post A Comment: