MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ametoa ripoti ya
ukaguzi wa hesabu ya mwaka 2014/15 iliyoibua kasoro nyingi kwenye
taasisi na mashirika mbalimbali ya serikali huku halmashauri zikibainika
kuwa na ‘madudu’ mengi.
Ripoti hiyo inaonesha kati ya halmashauri
164 zilizokaguliwa, 47 pekee ndizo zimepata hati safi, nyingine
zilizobakia zina hati zenye mashaka, zisizoridhisha na chafu. Kwa upande
wa mashirika ambayo ripoti hiyo imeyagusa, Shirika la Usafiri Dar es
Salaam (UDA) limebainika mauzo ya hisa zake yalikuwa batili, hivyo CAG
ameshauri lirudi chini ya usimamizi wa serikali hadi hapo mgogoro wa
mgawanyo wa hisa utakapotatuliwa.
UTATA JUU YA DART
Kuhusu
Wakala wa Usafiri wa Mwendo wa Haraka Dar es Salaam (DART), ripoti ya
CAG imebaini kuwa kwa mwaka wa fedha 2014/15 wakala huyo aliingia
mkataba na UDA-RT wa kutoa huduma ya usafiri wa mpito wa kuendesha
mabasi 76 kulingana na vigezo vilivyoainishwa kwenye mkataba.
Lakini,
Sheria ya Manunuzi ya Umma, mkataba huo ulitoa ongezeko la ununuzi wa
mabasi na kufikia 84 ili kulingana na matakwa ya DART. Hata hivyo kwenye
ukaguzi wa hesabu zao, CAG alibaini kuwepo na ununuzi wa mabasi 140
ambayo ni sawa na ongezeko la mabasi 56 yasiyo ndani ya mkataba.
WATUMISHI HEWA NA MISAMAHA YA KODI
Aidha,
ripoti hiyo imepigilia msumari kwenye suala la watumishi hewa na kusema
tatizo hilo limekuwa sugu na serikali za mitaa zinaongoza kwa kulipa
mishahara watumishi waliofariki na waliotoroka huku Sh bilioni 2.7
zikiwa zimetumika mwaka wa fedha 2014/15 kwa malipo hayo.
Jambo
lingine ambalo limejitokeza kwenye ripoti ya CAG, ni utoaji wa misamaha
ya kodi kwa kiwango cha juu huku ikionesha Sh trilioni 1.6 sawa na
asilimia mbili ya pato la ndani la taifa, zilisamehewa katika kipindi
kilichoishia Juni 30, 2015.
MADUDU KATIKA HALMASHAURI
Alisema
kwa mwaka unaoishia Juni 30 ,2015, jumla ya hati za ukaguzi 465
zilitolewa kwa Serikali Kuu, Serikali za Mitaa na mashirika ya umma.
Ripoti imeonesha kuwa mashirika ya umma na Serikali Kuu yamefanya vizuri
kwa kupata hati nyingi safi, huku zile za mashaka zikiwa chache.
Aidha
hakuna hati mbaya wala isiyoridhisha. Akifafanua alisema katika ukaguzi
huo, halmashauri ndizo zinaongoza kwa kufanya vibaya . Kati ya
halmashauri 164 zilizokaguliwa, 47 pekee ndizo zimepata hati safi,
nyingine zilizobakia ni zenye mashaka, zisizoridhisha na chafu.
MISAMAHA YA KODI
Wakati
huo huo, akizungumzia misamaha ya kodi kwa kipindi kilichoishia Juni
30, 2015, Profesa Assad alisema ripoti yao inaonesha kuwa kiasi cha
misamaha kilichotolewa ni Sh trilioni 1.6 sawa na asilimia mbili ya pato
la ndani la taifa.
Kiwango hicho kwa mujibu wa Profesa Asaad, ni
cha juu ikilinganishwa na lengo la serikali la kupunguza misamaha hiyo
isizidi asilimia moja ya pato la taifa.
Katika misamaha hiyo,
pia kuna utata kwenye mafuta yenye dhamana ya kodi ya Sh bilioni tano
ambayo yalionekana kwenye mfumo wa forodha wa (TANCIS) kuwa
yamesafirishwa nje kupitia nchini lakini hakuna ushahidi wa hilo.
DENI LA TAIFA
Akizungumzia
deni la taifa, Profesa Asaad alisema hadi kufikia Juni 30, mwaka 2015,
deni la taifa lilikuwa Sh trilioni 33.54. Deni la ndani lilikuwa Sh
trilioni 7.99 na deni la nje likiwa Sh trilioni 25.5 hivyo jumla ya deni
lote likiongezeka kwa asilimia 27 ikilinganishwa na deni lililoishia
Juni 30, mwaka 2014,hivyo ameishauri Serikali kuongeza jitihada za
kukusanya kodi ili kulipa madeni.
DOWNLOAD
APP YETU YA SWAHIBA NEWS ILI UWEZE KUPATA HABARI ZOTE MOJA KWA MOJA
KUPITIA SIMU YAKO YA MKONONI BILA KUINGIA KWENYE WEBSITE,KUDOWNLOAD
BONYEZA HAPA
Post A Comment: