MWANAMKE mkazi wa Mlimwa katika Manispaa ya Dodoma, Fatuma Mohamed
(39), anashikiliwa na Polisi kwa tuhuma za kumuua mtoto wa mke mwenzake,
kisha kumtumbukiza mwili wake kwenye karo la maji.
Mtoto aliyeuawa, Subira Ganyara mwenye umri wa mwaka mmoja, aliibwa
Aprili 19 nyumbani kwa mama yake mzazi, Agnes Yohana saa 3:00 usiku
wakati akiwa amelala chumbani, wakati mama yake akiongea nje na wenzake.
Mtoto huyo alipatikana Aprili 20, alfajiri akiwa amenyongwa na
kutumbukizwa kwenye karo la maji lililokuwa wazi.
Akielezea tukio hilo, baba wa mtoto huyo, Prosper Ganyara alisema
mtoto aliyeuawa alizaliwa Machi 23, 2015. Alisema, mtuhumiwa ni mkewe
waliyebahatika kupata watoto watatu, Kabuche Ganyara (13), Ganyara
Ganyara (11) na Msafiri Ganyara (7).
Alisema, alifunga ndoa ya Kiislamu na mwanamke huyo lakini hata hivyo
ndoa hiyo ilivunjika mwaka 2013 baada ya kukosa maelewano, ndipo
alipoanza kudai mahakamani haki ya kuchukua watoto wake ili awatunze
lakini, baada ya kesi hiyo kusikilizwa Mahakama ilimpa Fatuma
(mtuhumiwa) haki ya kutunza watoto wake.
Alisema, aliamua kukata rufaa Mahakama ya Mkoa Januari mwaka huu ili
apate haki ya kulea watoto wake na sasa kesi hiyo bado iko mahakamani.
“Mimi nikapata mwanamke mwingine Agness (mama wa mtoto aliyeuawa)
nikaenda kwao kujitambulisha na wakati huo yatari alikuwa mjamzito
tukakubaliana aendelee kukaa kwa wazazi wake na mimi nitatoa matunzo
yote,” alisema baba wa mtoto huyo.
Alisema juzi kati ya saa 2.30 usiku, mama wa Subira alikuwa amekaa
pembeni ya nyumba yao akiwa anaongea na wenzake, baada ya mazungumzo
aliingia ndani akakuta mtoto hayupo akawauliza majirani wakasema
hawajui.
“Wakaanza msako wa kutafuta mtoto usiku ule ule na alipoulizwa ni
nani anaweza kuhusika akasema ni mke mkubwa kwani mara nyingi amekuwa
akimtolea maneno ya vitisho kuwa kama asipokufa yeye atakufa mtoto,”
Gunyara alikariri maneno ya mzazi mwenzake na kukiri hata yeye aliwahi
kutolewa maneno hayo.
Pia alisema Fatuma aliwahi kumfuata mama mzazi wa Agness, Esther
Udoba akilalamika kuwa mtoto wake ameolewa na mume wake na hivyo ni heri
waachane kwani atamuua.
“Hata baba mzazi wa Agness aliwahi kumtolea maneno mazito na kumtolea
matusi, nikamshauri akirudia tena atoe taarifa Polisi na mimi nitakuja
na nakala ya talaka kama kielelezo kuwa tayari nilikuwa nimeachana na
mwanamke huyo,” alisema mwanamume huyo.
Alisema walipanga wakutane
wazazi wa Agness, Agness, Fatuma na yeye lakini kabla ya hilo
halijafanyika ndio tukio hilo limetokea.
Post A Comment: