WAKATI Bodi ya Shirika la Changamoto za Milenia (MCC) ikitangaza
kuinyima Tanzania msaada wa Dola za Marekani 473 (zaidi ya Sh trilioni
1), Serikali imesema ilishajiandaa kuhusu hatua hizo na fedha hizo
haikuzijumuisha katika bajeti ya mwaka ujao wa fedha wa 2016/17.
MCC imezuia fedha hizo za maendeleo kutokana na hatua ya Tanzania
kuitisha uchaguzi wa marudio ya Zanzibar pamoja na kutumika kwa Sheria
ya Makosa ya Mitandao. Chini ya Mpango wa Uwekezaji wa MCC–2, fedha hizo
zilikuwa ziende katika kuboresha huduma za umeme, ikiwamo kusambaza
umeme katika vijiji vingi zaidi nchini.
Kiasi cha asilimia 46 ya Watanzania kwa sasa wanapata umeme kutoka
asilimia 10 ya mwaka 2005 na sehemu kubwa ya asilimia hiyo ilitokana na
msaada wa MCC-1. Fedha hizo zilikuwa ni awamu ya pili ya msaada kutoka
MCC na tayari katika awamu ya kwanza, Tanzania ilipokea Dola za Marekani
milioni 698 ambazo zilitumika kwa ajili ya ujenzi wa barabara za
Tunduma- Sumbawanga, Tanga-Horohoro na Namtumbo-Songea-Mbinga.
Fedha hizo zilitumika kujenga upya mfumo wa huduma za maji kwa ajili
ya miji ya Dar es Salaam na Morogoro na zilitumika kusambaza umeme
katika vijiji vya mikoa 10 ya Tanzania Bara, zilitumika kutandaza njia
ya pili ya kusafirisha umeme chini ya Bahari ya Hindi kati ya Bara na
Tanzania Visiwani na pia zilitumika kujenga barabara zote kuu za Kisiwa
cha Pemba na baadhi ya barabara za Unguja kwa kiwango cha lami.
Akizungumzia jana, Waziri wa
Fedha na Mipango, Dk Phillip Mpango alisema tangu Desemba mwaka jana
walishasoma alama za nyakati na hivyo kuamua kutozijumuisha fedha za
MCC-2 katika maandalizi ya Bajeti ya Serikali yanayoendelea kwa mwaka
ujao wa fedha.
“Tulisoma kwenye mitandao matamshi ya viongozi wa Mfuko huo ndio
maana tukaamua kutozijumuisha fedha za MCC kwenye bajeti ya mwaka ujao
wa fedha, hivyo Watanzania wasiwe na wasiwasi juu ya kusitishwa kwa
msaada huo,” alisema Dk Mpango.
Hata hivyo, alisema Serikali itatoa tamko rasmi baada ya kupata barua
kutoka MCC ikiwaeleza wamesimamisha msaada huo hadi lini na nini
Tanzania inatakiwa kufanya ili kupata msaada huo. “Sisi tukipata hiyo
barua tutaitafakari na tutawajibu,” aliongeza waziri. Alisema Serikali
bado inaamini uhusiano wa Tanzania na Marekani ni mzuri na wa muda mrefu
hivyo huko mbele kutakuwepo na maelewano na fedha hizo zitatolewa.
Post A Comment: