WATU watatu wamekufa mkoani Kagera kwa matukio tofauti, akiwemo aliyepigwa hadi kufa na mumewe kutokana na ugomvi wa kifamilia.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Augustine Ollomi alisema tukio la
kwanza lilitokea Machi 27, mwaka huu katika Kata ya Ijumbi wilayani
Muleba, ambako mwanamke Georgina Emmanuely (68) alikutwa ameuawa kwa
kupigwa na kitu chenye ncha kali kichwani na mwili wake kutelekezwa
shambani mwa Felician Andrew.
Alisema mwili wa marehemu umechukuliwa na ndugu zake na kufanya maziko baada ya kufanyiwa uchunguzi.
Alisema wanamshikilia Johansen Sebastian (39) kwa mahojiano zaidi
kuhusu tukio hilo, ambalo polisi wanaendelea na uchunguzi wa kina ili
kuwanasa wahusika wengine ili wachukuliwe hatua za kisheria.
Katika tukio la pili, Kamanda Ollomi alisema lilitokea Machi 27,
mwaka huu Kijiji cha Nyamihaga wilayani Ngara ambako mwanamke Janeth
Abyalimana (36) ameuawa na mume baada ya kumpiga kwa mateke na ngumi
sehemu mbalimbali za mwili wake na kupata majeraha makubwa, kutokwa damu
nyingi na kusababisha kifo.
Alisema mtuhumiwa, Alfonce Abyalimana, alipoona kasababisha kifo
hicho, alikimbia na polisi wanaendelea na msako mkali wa kumtafuta ili
afikishwe kwenye vyombo vya sheria kujibu tuhuma hiyo.
Alitaja tukio jingine lililotokea Machi 28, mwaka huu katika eneo la
Kemondo Bukoba Vijijini, ambako mtembea kwa miguu, Gabriel William( 60)
aligongwa na gari na kufa papo hapo, ambako gari hilo halikufahamika
namba kwani ilikuwa usiku wakati akijaribu kuvuka barabara ya Muleba -
Kemondo na kisha lilitokomea kusikojulikana.
Alisema wanaendelea kumsaka mwendesha gari hilo ili apambane na mkono wa sheria.
Post A Comment: