Mchungaji Peter Msingwa,Waziri kivuli wa mambo ya nnje |
Nimesikitishwa na Tanzania kukosa fedha za MCC ambazo zilikuwa ni
muhimu sana katika kuharakisha upatikanaji wa umeme kwa Watanzania wa
vijijini. Hata hivyo, ningependa kuweka wazi kuwa Tanzania haijaonewa
hata kidogo kunyimwa msaada wa Shilingi Trilioni Moja na Shirika la
Misaada la Marekani la MCC kama ilivyopotoshwa na Serikali.
Kauli ya
Waziri wa Mambo Nje, Balozi Agustine Mahiga, ya kuelezea “kushitushwa na
kusikitishwa” na uamuzi wa Bodi ya MCC kusitisha msaada na mahusiano
yake na Tanzania, ni kauli isiyo ya kidiplomasia, ya kinafiki na
inayopaswa kupingwa kwa nguvu zote na kila Mtanzania mwenye kujali
kujali utu, demokrasia, utawala bora na ushirikiano mwema baina ya Nchi
hii na mataifa mengine.
Nikiwa ni Waziri wa Mambo Nje napinga upotoshwaji na utetezi uliotolewa na Serikali kwasababu zifuatazo;
1. Ni vema ikazingatiwa kuwa MCC inazingatia vigezo 17 katika kuchagua nchi inayostahili kupata msaada na miongoni mwa vigezo vya msingi kabisa ni nchi husika kuwa na dhamira ya dhati ya kuimarisha demokrasia na kuendesha chaguzi zilizo huru na haki
. Na katika taarifa yake MCC
ilieleza maeneo ambayo Tanzania imekiuka vigezo kuwa ni marudio ya
uchaguzi haramu wa urais Zanzibar na kupitisha Sheria ya Makosa ya
Mawasiliano ya Mitandaoni –“Cyber Crime”, sheria inayonyima uhuru wa wa
kujieleza na uhuru wa kujumuika; nanukuu:
“Serikali ya Tanzania haijachukua hatua za kuhakikisha kuheshimiwa
kwa uhuru wa kujieleza na uhuru wa kujumuika katika utekelezwaji wa
sheria ya Uhalifu wa Mtandao.”
“Tanzania iliendelea na uchaguzi wa marudio Zanzibar ambao
haukushirikisha wote na wala haukuakisi maoni ya wote, licha ya
malalamiko kutoka kwa serikali ya Marekani na jamii ya kimataifa”,
mwisho wa kunukuu.
Kwa mantiki hii, ni dhahiri kuwa Tanzania haikupaswa “kushitushwa” na
uamuzi wa MCC. Serikali ilivifahamu vizuri na mapema vigezo vya
kustahili kupewa misaada na MCC. Inashangaza na kusikitisha kuona Msomi
na Mwanadiplomasia mzoefu kama Balozi Mahiga akilitia Taifa “Aibu ya
Mwaka” kwa kulalamikia “kuonewa” na kutoa kauli za “hovyo” kama
alivyozitoa.
Kauli ya Waziri Mahiga, za kukataa kukiri makosa yaliyo dhahiri
yaliyofanywa na Serikali na Chama Chake (CCM), zinaweza kabisa kuuweka
rehani uhusiano na ushirikiano mzuri wa kidiplomasia ambao Tanzania
imekuwa ikiupata kutoka kwa nchi mbalimbali na mashirika ya kimataifa
kama MCC.
Tukiweka mbele maslahi ya nchi hii yakiwemo ya kudumisha
mahusiano mazuri ya kimaendeleo na nchi nyingine, Kambi rasmi ya
Upinzani tunaiomba MCC, Marekani na mataifa mengine kuzipuuza kauli za
hovyo zilizotolewa na Waziri Mahiga, kwani haziakisi ustaarabu wa
Watanzania.
2. Pili, Tanzania si Mbia mgeni kwa MCC. Tanzania ilishapokea awamu
ya kwanza ya fedha za msaada kutoka MCC ambazo zilikuwa ni Dola za
Marekani milioni 698. Fedha hizi zilitumika kwa ajili ya ujenzi wa
barabara za Tunduma- Sumbawanga, Tanga-Horohoro na
Namtumbo-Songea-Mbinga.
Zilitumika pia kujenga upya mfumo wa huduma za
maji kwa ajili ya miji ya Dar es Salaam na Morogoro na kusambaza umeme
katika vijiji vya mikoa 10 ya Tanzania Bara. Zilitumika kutandaza njia
ya pili ya kusafirisha umeme chini ya Bahari ya Hindi kati ya Bara na
Tanzania Visiwani na kujenga barabara zote kuu za Kisiwa cha Pemba na
baadhi ya barabara za Unguja kwa kiwango cha lami.
Kwa namna yoyote ile
isingewezekana kwa MCC walewale kuionea Tanzania ile ile waliyoisaidia
katika awamu ya kwanza ya misaada yao. Ni dhahiri kuwa Nchi imepoteza
sifa kwasababu zilizoelezwa – na kimsingi sababu zenyewe ni uchu na
ulevi wa madaraka uliopitiliza unaofanywa na Chama Cha Mapinduzi (CCM)
na Serikali yake.
Hatua ya MCC kusitisha uhusiano na Tanzania ni ushahidi tosha kuwa
hujuma za uchaguzi na ukiukwaji mkubwa wa demokrasia na utawala bora,
unaofanywa na serikali ya CCM na ambao Wapinzani tumekuwa tukiulalamikia
mara kwa mara sasa umefikia hatua mbaya zaidi kiasi cha kugusa hisia za
jumuiya ya kimataifa.
Ni mtazamo wangu kuwa MCC na jumuiya ya kimataifa bado walichelewa
sana kugundua “udhalimu” wa Serikali ya CCM, ambayo karibu mara zote
imekuwa ikihujumu haki na uhuru wa watu kwenye chaguzi, na si kwa upande
wa Zanzibar tu, bali pia na uchaguzi wa Jamhuri ya Muungano.
Sheria
kandamizi zilizopo Tanzania si hiyo ya “Cyber Crime” tu. Tume ya Jaji
Francis Nyalali ilibainisha Sheria nyingi kandamizi na kushauri
zifanyiwe mapitio ya kuziboresha lakini hadi leo “serikali isiyo ya
kidemokrasia ya CCM” imeendelea kuzidumisha sheria hizo na kuongeza
nyingine kama hii ya “Cyber Crime”.
Natoa rai kwa jumuiya ya kimataifa
kutokukubali kurubuniwa tena na serikali ya CCM na badala yake
ishirikiane kwa karibu na Watanzania wote wazalendo katika kuboresha
misingi ya utawala bora na demokrasia kwenye nchi hii.
3. Tatu, mabalozi wa nchi mbalimbali washirika wa maendeleo ikiwemo
Marekani, walishatoa rai zaidi ya mara moja wakiionya na kuishauri
Serikali ya Rais Kikwete na baadaye Rais Magufuli kuchukua hatua za
kuutatua mgogoro wa uchaguzi wa Zanzibar.
Aidha, walishauri mara kadhaa
kuwa uchaguzi wa marudio usingeweza kuwa suluhu halali ya kumaliza
tatizo la Zanzibar. Badala ya kuchukua hatua hasa za kukisihi Chama
chake kuheshimu maamuzi halali ya wapiga kura wa Zanzibar yaliyofanywa
Oktoba 25 mwaka jana, Rais wa Jamhuri ya Muungano, John Magufuli,
alipuuza rai zote hizo na kwa kiburi cha hali ya juu alisema “hahusiki
na suala la Zanzibar”.
Mbali na Mabalozi hao, hata aliyekuwa Waziri wa Mambo Nje wa Serikali
ya Awamu ya Nne, Bernard Membe, alionya na kutoa tahadhari kuhusu suala
la Zanzibar lilivyokuwa likichukuliwa kwa mzaha-mzaha, badala ya
kutatuliwa kwa umakini.
Matokeo yake ndiyo haya ya kutengwa na MCC.
Inasikitisha kuona Serikali ya Magufuli ikiwa na uweledi finyu katika
medani ya diplomasia ya kimataifa na kuupuza nchi rafiki.
Uamuzi wa MCC unapaswa kuchukuliwa kwa tahadhari kubwa na Serikali.
Nchi nyingi rafiki ni nchi zinazosimamia misingi ya utawala bora na
demokrasia na zilishaonyaonyesha kutoridhishwa na suala la Zanzibar na
Sheria ya Cyber Crime.
Naonya kuwa upo uwezekano kwa nchi wahisani, kila
moja kwa nafasi yake, kuchukua uamuzi kama uliochukuliwa na MCC wa
kusitisha ushirikiano wa kimaendeleo na Tanzania, kama hatua za dharura
hazitachukuliwa kurekebisha hali ya mambo
USHAURI KWA SERIKALI
Kambi rasmi ya Upinzani siku zote tumekuwa msitari wa mbele kuitaka serikali na vyombo vyake ijenge uwezo endelevu wa kujitegemea. Hata hivyo, ni ukweli ulio dhahiri kuwa wakati tukijenga uwezo wa kujitegemea, bado tunahitaji kuutumia vizuri ushirikiano wa kutegemeana na nchi rafiki na mashirika ya kimataifa. Tanzania haiwezi kuishi kama Kisiwa, hii ni Dunia ya kuhitajiana.
Trilioni Moja za MCC ni muhimu katika kuharakisha usambazaji umeme vijijini. Tanzania inataka kufikia hadhi ya kuwa nchi yenye uchumi wa kiwango cha kati kama ilivyo India na Malaysia ifikapo mwaka 2025 kwa mujibu wa Dira ya Taifa. Nchi hizi tunazotaka kuzifikia nazo zinajenga uwezo zaidi wa kimaendeleo kwa kutegemeana pia na nchi na washirika wengine wa kimaendeleo. Serikali isijifanye haitaki misaada wakati ukweli ni kuwa bado Bajeti yetu ya nchi inahitaji kusaidiwa na nchi rafiki. Ni wakati wa Serikali kuacha kauli za hovyo na kuchukua maamuzi magumu ya kujirekebisha kama ifuatavyo.
1. Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Dr. Mohamed Shein wanapaswa kuonyesha kuwa wanawapenda zaidi Watanzania kuliko wanavyovipenda vyeo vyao vya kulazimisha. Dk Shein akatae kuburuzwa, akatae kuanzia sasa kubeba laana ya dhuluma na kusababisha Tanzania na Zanzibar zitengwe.
Namshauri
achukue uamuzi wa kishujaa wa kujiuzulu urais haramu wa Zanzibar, ili
apishe mazungumzo mapya ya kutafuta muafaka Zanzibar.
2. Serikali ilete muswada Bungeni wa kurekebisha Sheria ya Makosa ya Mitandaoni na Sheria nyingine zote kandamizi kama zilivyoainishwa na Tume ya Jaji Nyalali.
3. Serikali ianze bila kuchelewa kutekeleza mchakato wa kupata Katiba Mpya kwa kuanzia pale ilipoishia Tume ya Jaji Warioba, vinginevyo naonya kuwa madai na kishindo kipya cha vuguvugu la Katiba Mpya ambalo Wapinzani tunakusudia kulianzisha upya, linaweza kuiweka Tanzania katika picha mbaya. Tunaitaka serikali itupe ushirikiano katika kujenga demokrasia na utawala bora kwenye nchi hii.
Post A Comment: