KAMPUNI inayojihusisha na ujenzi wa miundombinu ya umeme katika mikoa
ya Mwanza na Tabora ya Chico CCC ya China, imepewa muda wa miezi miwili
ya kuhakikisha imekamilisha miradi yake ya umeme.
Agizo hilo limetolewa na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa
Sospeter Muhongo alipokutana na kampuni hiyo ofisini kwake Dar es Salaam
kwa ajili ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa miradi yake ya umeme
vijijini. Kampuni hiyo inatekeleza miradi ya umeme inayosimamiwa na
Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
Mara baada ya kupokea taarifa hiyo na kutoridhishwa na kasi ya
utekelezaji wa miradi ya kampuni hiyo, Profesa Muhongo aliitaka kampuni
hiyo kuhakikisha inakamilisha miradi yake ifikapo mapema Mei mwaka huu.
Alisisitiza kuwa wananchi wanahitaji umeme wa uhakika, ambao ni nguzo
ya ukuaji wa uchumi wa nchi kupitia viwanda, hivyo serikali haitamwonea
haya mwekezaji yeyote asiyetekeleza mradi wa umeme aliopewa kwa kasi
inayoridhishwa.
Post A Comment: