YANGA na Azam leo zinashuka kwenye viwanja tofauti katika michezo ya Kombe la Shirikisho hatua ya robo fainali.
Michuano hiyo inayojulikana pia kama Kombe la FA imeingia hatua ya
robo fainali, ambapo Jumamosi iliyopita timu ya Mwadui iliifunga Geita
Gold Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza mabao 3-0 na kufuzu nusu fainali.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Shirikisho la Soka Tanzania
(TFF), Yanga itacheza Uwanja wa Taifa Dar es Salaam ikiwa mwenyeji wa
Ndanda FC ya Mtwara, wakati Azam FC itakuwa Uwanja wa Azam Chamazi
kuivaa Prisons.
Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) linatarajiwa
kuendelea Alhamisi kwa michezo miwili kuchezwa katika hatua ya robo
fainali ya michuano hiyo. Mechi zote zinatarajiwa kuwa na upinzani wa
hali ya juu, huku kila timu ikipania kushinda na kufuzu nusu fainali.
Bingwa wa michuano hiyo atawakilisha nchi katika michuano ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika (CAF CC) mwaka 2017.
Yanga na Azam pia zitatumia michezo hiyo kama maandalizi yao kwa
ajili ya mechi za kimataifa mwishoni mwa wiki ijayo, ambapo Azam
itacheza na Esperance ya Tunisia na Yanga itacheza na Al Ahly ya Misri.
Pia mechi ya leo ni maandalizi ya michezo ya viporo vya Ligi Kuu
Tanzania Bara, ambapo Yanga na Azam zitacheza kuanzia Jumamosi wiki hii.
Robo fainali nyingine ya michuano hiyo itakuwa Aprili 9 mwaka huu,
wakati Simba itakapokuwa mwenyeji wa Coastal Union ya Tanga Uwanja wa
Taifa, Dar es Salaam.
Post A Comment: