RAIS Mteule wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein anaapishwa leo kwenye
Uwanja wa Amaan mjini hapa. Kuapishwa kwa Dk Shein kunamfanya apate
fursa nyingine ya kuongoza Zanzibar kwa muda wa miaka mitano ijayo,
baada ya mgombea huyo wa CCM kushinda urais wa Jumapili kwa kujinyakulia
asilimia 91 ya kura zilizopigwa.
Serikali pia imetangaza kuwa leo pia ni siku ya mapumziko visiwani
hapa ili kuwapa fursa wananchi wahudhurie sherehe za kuapishwa kwa
kiongozi wao. Wageni ambao wanatarajia kuhudhuria kwenye sherehe hizo
ambazo zitaanza saa 2 asubuhi ni Rais John Magufuli na viongozi wengine
wa ngazi ya juu wa kitaifa wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud
alithibitisha kuwepo kwa viongozi hao akiwemo Makamu wa Rais, Samia
Suluhu Hassan, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na mawaziri wa Serikali ya
Muungano katika shughuli ya kuapa kwa Rais mteule Dk Shein.
Wakati Rais anaapishwa leo, amani na utulivu bado ni mkubwa visiwani
hapa licha ya kuwa ulinzi umeendelea kuimarishwa katika maeneo
mbalimbali nyeti na mitaani. Baadhi ya shughuli za kiuchumi kama maduka
yameanza kufunguliwa jana, hali inaonesha kuwa utulivu upo wa kutosha
kama ambavyo Serikal iliahidi kuwa itahakikisha amani inakuwepo visiwani
hapa.
Dk Shein wa CCM anaenda kuongoza katika miaka mitano ijayo katikati
ya mpasuko wa kisiasa uliopo visiwani hapa kutokana na Chama cha
Wananchi (CUF) ambacho ni chama kikuu cha upinzani kususa kushiriki
kwenye uchaguzi wa marudio ambao ulifanyika Jumapili iliyopita.
Tayari CUF wameshatangaza kuwa hawautambui ushindi huo wa Dk Shein
kwa kile wanachoeleza kuwa umetokana na uchaguzi haramu baada ya
demokrasia kubakwa kwani wananchi wa Zanzibar walishaamua kwenye
uchaguzi wa Oktoba 25, 2015.
Chama hicho kimeahidi kuendelea kudai haki yake kwa amani na
kimewataka wananchi kuendelea kuitunza amani iliyopo na watakuwa
wanapatiwa taarifa za hatua itakayofikia chama hicho katika harakati za
kudai haki. Kwa ujumla wananchi wa Zanzibar kuanzia juzi wanaonekana
wamoja na kwa kuwa ulinzi uliopo unawakataza kukaa kwenye makundi.
Post A Comment: